Saturday 11 February 2012

STORY MANYARA


Joseph Lyimo,Babati
ASKARI wa JESHI la polisi mkoani Manyara amedaiwa kusababisha kifo cha mwendesha pikipiki wa kubeba abiria (bodaboda) baada ya kutokea ajali ya kugongana wakati akimfukuza na pikipiki ya Halmashauri ya wilaya ya Babati mwendesha bodaboda huyo.

Mwendesha pikipiki huyo Hussein Jumanne (28) mkazi wa Nyungu wilayani Babati,aligongana na askari polisi huyo Koplo Emmanuel ambaye pia alijeruhiwa vibaya na hadi hivi sasa amelazwa kwenye hospitali ya rufaa ya KCMC ya mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo,mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa chanzo cha ajali hiyo iliyosababisha kifo ni kukimbizana kati ya askari polisi huyo na mwendesha pikipiki huyo anayedaiwa kuwa alikuwa amebeba dawa za kulevya aina ya mirungi.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kutokea kwa tukio hilo mashuhuda hao walidai kuwa askari huyo alikuwa anaendesha pikipiki hiyo mali ya halmashauri ya Babati na alikuwa anamkimbiza mwendesha pikipiki huyo akidaiwa kubeba mirungi.

“Askari alikuwa ameazima pikipiki ya Halmashauri na akawa anamkimbiza mwendesha pikipiki huyo ambaye inadaiwa alikataa kusimama kutokana na kuwa alibeba mirungi hivyo waligongana baada ya kumzuia kwa mbele,” walisema.

Walidai kuwa baada ya kukataa kusimama askari huyo alimkimbiza na alipomkuta alimpita kwa ghafla na kumzuia mwendesha bodaboda ambaye aliigonga pikipiki hiyo iliyokuwa kwenye mwendo wa kasi kubwa.

“Baada ya ajali hiyo wote wawili walipoteza fahamu na kukimbizwa hospitali ya KCMC na Jumanne akafariki dunia alipofikishwa hospitalini hapo na koplo Emmanuel hali yake bado ni mbaya,” walisema.

Hata hivyo,Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara,Kamishna msaidizi,Liberatus Sabas alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 6:30 usiku kwenye barabara kuu ya Babati-Dodoma.

Kamanda Sabas alisema askari huyo alikuwa anaendesha pikipiki aina ya Honda yenye namba za usajili SM 9426 na Jumanne alikuwa anaendesha pikipiki yenye namba za usajili T116 BNQ.

Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa kwenye hospitali ya KCMC mjini Moshi kwa uchunguzi zaidi na askari huyo anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.    

MWISHO.

Joseph Lyimo,Babati
OFISA Mtendaji wa Kijiji cha Arri Wilayani Babati,Mkoa wa Manyara,Emmanuel Sanka,ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alifungiwa ofisi na wananchi wa kijiji hicho kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma amesimamishwa kazi.

Akithibitisha kusimamishwa kazi mtendaji huyo,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati,Chediel Mrutu,alisema Sanka amesimamishwa kazi hadi hapo uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili utakapokamilika.

Mrutu alisema Ofisa mtendaji huyo wa kijiji cha Arri ataendelea kupokea nusu mshahara wake hadi hapo uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika baada ya halmashauri hiyo kuunda tume ya kuchunguza jambo hilo.

Hivi karibuni wakazi wa kijiji hicho walimfukuza Ofisa mtendaji huyo ofisini kwake na pia waliifunga ofisi yake kwa kufuli wakimtuhumu Sanka kwa ubadhirifu wa fedha za kijiji hicho cha Arri.

Pia wananchi hao walidai kuwa wanamtuhumu Sanka kwa kutowasomea mapato na matumizi ya kijiji hicho kwa muda wa miaka mitatu mfululizo hali iliyowafanya washindwe kujua mchanganuo wa fedha za kijiji chao.

Waliupongeza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Babati vijijini kwa kumsimamisha kazi Ofisa mtendaji huyo wa kijiji na kumchunguza kutokana na kudaiwa kufanya ubadhirifu huo na kutowasomea mapato na matumizi ya kijiji.

Walisema hatua za kisheria zichukue mkondo wake dhidi ya mtendaji huyo ili iwe funzo kwa watendaji wengine wenye tabia kama za Ofisa huyo za ubadhirifu na ufujaji wa fedha za umma.

“Huyu Ofisa mtendaji hakuwa na nidhamu ya kazi kwani mara nyingi alikuwa anafunga ofisi na kushindwa kuwahudumia wananchi hivyo kuigeuza ofisi yetu kuwa mali yake binafsi kwa kufanya anavyotaka yeye,” walisema wanakijiji hao.

Walidai kuwa Ofisa mtendaji huyo mara nyingi alikuwa anafunga ofisi hiyo kwani alikuwa anaifungua saa 10 jioni na kuifunga saa 1 usiku hivyo kujigeuza mfalme wa eneo hilo kwa kujiamulia kila kitu peke yake.

Matukio ya watendaji wa vijiji hapa nchini kutowasomea wanavijiji mapato na matumizi ya kijiji yamekithiri sehemu nyingi baada ya watendaji hao kujigeuza miungu watu kwa kujiamulia kila kitu hivyo kurudisha nyuma maendeleo yao.      

MWISHO.


Joseph Lyimo,Simanjiro
WATUMISHI watano wa idara ya maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Langai wamefikishwa Mahakama ya wilaya ya Kiteto kwa kosa la wizi na kuchoma nyumba za wakulima 16 wa kitongoji cha Najuu wilayani humo.

Watumishi hao wakiongozwa na Ofisa wanyamapori wa wilaya hiyo Titus Towo (32) na Mwenyekiti huyo wa kitongoji cha Langai Jacob Andrew (37) walifikishwa kwenye Mahakama ya wilaya ya Kiteto mbele ya Hakimu Mfawidhi Nestory Baro.

Akisoma hati ya mashtaka ya kesi hiyo juzi,kwenye mahakama hiyo,Mwendesha mashtaka wa polisi,Inspekta Paul Kimaro aliwataja washtakiwa wengine ni Jatani Mollel (35),Khalifa Nyela (42) na Ndetaulo Kitomary (50) wakazi wa mji mdogo wa Orkesumet.

Katika kesi hiyo ya namba 37/2012,Kimaro alidai washtakiwa hao wanatuhumiwa kutenda makosa hayo ya kuchoma nyumba na wizi wa mali za wakulima 16 wa kitongoji cha Najuu,kijiji cha Langai huku wakitambua kufanya hivyo ni kosa na kinyume cha sheria.

Mwendesha mashtaka huyo alisema kwamba washtakiwa hao bila halali wanadaiwa kutenda makosa hayo Januari 30 mwaka huu saa 9 alasiri kwenye eneo la mashamba ya Kitongoji cha Najuu katika kijiji hicho cha Langai.

Alidai kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kuchoma moto makazi hayo na wizi wa baiskeli mbili,majembe na mapanga na kusababisha hasara ya mali hizo zenye thamani ya sh2,746,000 milioni mali ya wakulima 16 wa kijiji hicho.

Hata hivyo,washtakiwa hao walipoulizwa mahakamani hapo kama ni kweli walitenda makosa hayo walikana na Hakimu Baro aliiahirisha kesi hiyo hadi Februari 14 mwaka huu itakapotajwa tena.

Baadhi ya wakulima hao wakizungumza na Mwananchi juzi walidai kuwa Mwenyekiti wa kijiji hicho naye anatakiwa kuunganishwa na washtakiwa hao kwani alishiriki kuchoma moto makazi yao.

“Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hata kama ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM wilaya ya Simanjiro,anatakiwa kuunganishwa kwenye kesi hii kwani naye alishiriki kutuchomea moto mali zetu na kutuathiri kiuchumi,” walisema. 

MWISHO.


No comments:

Post a Comment