Friday, 16 March 2018

ZAHANATI GALANGAL YAZINDULIWA


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza na wananchi wa Kata ya Bassotu juu ya tatizo la uvuvi haramu kwenye bwawa la Bassotu.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bassotu A, Wilayani Hanang' Samson Sima (Chadema) akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na kujiuzulu nafasi hiyo kwa kuondoka Chadema na kujiunga na CCM.


Zahanati ya Galangal yazinduliwa

Wananchi 8,400 wa Kijiji cha Galangal Wilayani Hanang' Mkoani Manyara, wanaotembelea umbali wa kilometa 15 kufuata huduma ya afya Kata ya Bassotu, wanatarajia kuondokana na adha hiyo baada ya zahanati yao kukamilika. 

Ujenzi wa zahanati hiyo umegharimu sh65.6 milioni, ambapo wananchi wamechangia sh32 milioni na halmashauri ya wilaya imechangia sh33.6 milioni. 

Kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Hanang, Jackoracha Daimon akizungumza jana alisema ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2017. 

Daimon alisema zahanati hiyo ina vyumba vya waganga, wauguzi, stoo ya dawa, chumba cha mama na mtoto, sehemu ya wajawazito kujifungulia na maabara. 

Alisema pamoja na kukamilika kwa jengo hilo kuna changamoto ya uhaba wa watumishi, nyumba za watumishi na kukoseka kwa huduma ya maji. 

Mkazi wa Kijiji cha Galangal, Ester Massay alisema kukamilika kwa zahanati hiyo kutamaliza kero ya muda mrefu ya kufuata huduma ya afya umbali mrefu.  

Massay alisema kwa sababu majengo ya zahanati hiyo yamekamilika inapaswa ianze kufanya kazi kwani wanawake na watoto ndiyo wamekuwa wakipata matatizo kwa kutembelea umbali mrefu. 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bryceson Kibassa kuhakikisha zahanati hiyo inaanza kutoa huduma mara moja ili wananchi hao wapate huduma ya afya kwa ukaribu zaidi. 

Mnyeti aliwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kuchanga fedha zao na serikali kuwaunga mkono kwa kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo. 

"Wananchi wengine waige mfano huu kwa kujenga zahanati hadi hatua ya rinta ndipo serikali itawaunga mkono kwa kumalizia kama ilivyofanya hapa Galangal," alisema. 

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya hiyo Kibassa alisema hadi mwezi Julai mwaka huu, zahanati hiyo itaanza kufanya kazi. 

Kibassa alisema wameshatenga nafasi za ajira mpya ili kukabiliana na hali ya upungufu wa watumishi vituoni ikiwemo uwezekano wa kufungua vituo vilivyokamilika. 

"Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi ina mpango wa ujenzi wa nyumba za watumishi katika zahanati na serikali ya kijiji ichangie ufikishaji wa maji eneo hilo," alisema. 



No comments:

Post a Comment