Friday 16 March 2018

MNYETI KUWASHUSHA VYEO WAKUU WA SHULE ZITAKAZOPATA ZIRO



Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akipokea heshima kutoka kwa skauti mara baada ya kuwasili Wilayani Hanang jana alipoanza ziara ya siku tano.



Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akiangalia kiatu kilichotengenezwa na kikundi cha Datoga cha Wilayani Hanang kinachotengenezwa vifaa vinavyotokana usindikaji wa ngozi. 




Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, (kushoto) akizungumza kwenye eneo la kuhifadhi dawa baada ya kukagua mazingira ya hospitali ya Wilaya ya Hanang kwenye ziara yake ya siku tano.

Mnyeti kuwashusha vyeo wakuu wa shule zitakazopata ziro Manyara


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesema atawashusha vyeo wakuu wote wa shule za sekondari ambao wanafunzi wao watapata daraja ziro kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne utakapofanyika mwaka huu. 

Hivi karibuni, Mnyeti aliagiza walimu wakuu 150 wa shule za msingi mkoani humo washushwe cheo baada ya Manyara kushika nafasi ya pili kutoka mwisho kwenye matokeo ya darasa la saba na wakashindwa kupata wastani wa asilimia 50. 

Akizungumza wilayani Hanang' Mnyeti alisema endapo hata mwanafunzi hata mmoja wa shule ya sekondari akipata ziro kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne atamshusha cheo mkuu wa shule. 

Alisema hatakubali kuona mkoa wake unakuwa nyuma kwenye suala la elimu kwani mazingira ya mikoa mingine ni sawa na Manyara hivyo hatakubali kuona wanafunzi wanashindwa kufaulu. 

"Kwa nini sisi Manyara tunakuwa watu wa mwisho kwenye kila kitu, nataka tuwe wa mwisho kwenye maambukizi ya virusi pekee hapa nchini siyo elimu," alisema Mnyeti. 

Alisema aliwachukulia hatua walimu wakuu 150 wa mkoa huo ambao shule zao hazikufanya vizuri kwenye mtihani wa darasa la saba kwa kuwashusha vyeo, sasa ni zamu ya wakuu wa shule za sekondari. 

"Kama wewe ni mkuu wa shule ya sekondari na mwanafunzi wa kidato cha nne hata mmoja akipata sifuri, wewe anza kuondoka mwenyewe kwenye nafasi hiyo," alisema Mnyeti. 

Alisema atashangazwa na kitendo cha mwanafunzi wa kidato cha nne kushindwa kupata alama C hata kwenye matokeo ya somo la kiswahili. 

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, George Bajuta alimpongeza Mnyeti kwa kuwachukulia hatua walimu wakuu wa shule za msingi zilizokuwa na chini ya wastani wa 50 kwenye matokeo ya darasa la saba.

Bajuta alisema Mnyeti ni kiongozi mchapakazi, anayechukua hatua mara moja hivyo hata kwenye uamuzi wa wakuu hao wanamuunga mkono kwa asilimia 100. 

"Umekuja hapa kwetu Manyara kwa muda mfupi wa miezi minne lakini kazi uliyofanya ya kutetea wanyonge na kutatua migogoro imekuwa kama miaka minne," alisema. 

Ofisa elimu wa halmashauri ya wilaya ya Hanang' Omari Maje alisema kiujumla walishika nafasi ya pili kimkoa kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka jana ila kwa shule za serikali pekee waliongoza kwa Manyara. 

"Mheshimiwa mkuu wa mkoa, kwa wanafunzi wa wilaya ya Hanang' wamejiandaa ipasavyo kufanya vizuri kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne unaotarajiwa kufanyika mwaka huu," alisema Maje. 






No comments:

Post a Comment