Katika kusherehekea wiki ya siku ya
wanawake duniani, wabunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara kwa tiketi ya CCM,
Martha Umbullah na Ester Mahawe, wametoa msaada wa sare za shule na vifaa vya
kuandikia kwa watoto yatima 43 wa shule ya msingi Bonga ya Mjini Babati.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Januari
Barnabas alisema kati ya wanafunzi hao yatima 43 wakiwemo wavulana 19 na
wasichana 24.
Ester Mahawe akizungumza wakati
wanakabidhi msaada huo wa sare za shule ikiwemo kaptula, mashati, sketi,
blauzi, masweta, viatu, maboksi mawili ya kalamu, madaftari na majaladio,
alisema umewagharimu sh1.6 milioni.
Mahawe alisema wametoa msaada kwa
yatima hao kwani jambo lililo bora hapa duniani ni kusaidia wahitaji ndiyo
sababu na wao wabunge wawili wakashirikiana kufanya hivyo.
"Ibada nzuri ni kusaidia
wahitaji hata sisi wakristo na waislamu tunaambiwa kuwa tuwe tunawasaidia
wenzetu na ndivyo tulivyofanya," alisema Mahawe.
Barnabas alisema wanakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo wanafunzi kutokula chakula cha mchana kwani nusu ya
wanafunzi wa shule hiyo wanakaa umbali wa zaidi ya kilometa mbili.
Alisema pia wanakabiliwa na
changamoto ya madarasa kwani yapo madarasa 15 na nyumba za walimu ni chache
kwani wapo 22 na nyumba zilizopo ni tano zilizochakaa.
Hata hivyo, Martha Umbullah alisema
changamoto ya wanafunzi kutokula shuleni inatakiwa ipatiwe ufumbuzi kwa
kuwekewa mikakati kwani siyo jambo zuri wanafunzi kurudi nyumbani mchana kwa
ajili ya kula.
Umbullah alisema viongozi wa eneo
hilo akiwemo diwani na kamati ya shule wanapaswa kukaa pamoja na wazazi ili
kufanikisha wanafunzi wapate chakula cha mchana shuleni.
"Japokuwa sisi siyo wabunge wa
jimbo hili, lakini ni wabunge wa viti maalum wa mkoa tunafanya kazi kwenye
wilaya zote tano na halmashauri saba zilizopo," alisema Umbullah.
Pia, msafara wa wabunge hao
ulioongozana na Mwenyekiti na katibu wa UWT wa mkoa huo, Venosa Mjema na Haynes
Munisi, ulitoa msaada wa vyakula kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Msafara huo ulitoa magunia 12 ya
mahindi, madebe 13 na nusu ya maharage, lita 60 za mafuta ya kupikia na
mwanafunzi mmoja wa darasa la pili kushonewa sare hadi ahitimu darasa la saba.
No comments:
Post a Comment