Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander
Mnyeti ameagiza wakala wa barabara za mijini na vijijini (Tarura),
kuwashirikisha viongozi wa maeneo husika pindi wanapotaka kuandaa bajeti za
barabara ili kutosababisha migongano ya kutotambulika barabara zinazopaswa kupewa
kipaumbele kwenye ukarabati na ujenzi.
Akizungumza jana mjini Babati kwenye
kikao cha bodi ya barabara ya Mkoa huo, Mnyeti alisema Tarura ni chombo cha
serikali hivyo wanatakiwa wawashirikishe viongozi wa maeneo husika ili kusiwepo
na migongano tofauti na sasa kwani wanajitenga.
Mnyeti alisema Tarura wasijigeuze
kuwa taasisi ya kipekee iliyopo serikali kuu ambayo haiwajibiki wilayani au
mkoani ili hali ni wajibu wao kutoa taarifa na kushiriki vikao.
"Hizo barabara siyo za kwenu,
sitaki kusikia mnapitisha barabara zijengwe ili hali viongozi wa wilaya hawajui
au mimi sijui, ninyi Tarura msigeuze taasisi kuwa ya kwenu," alisema
Mnyeti.
Alisema kwenye mkoa wake hataki
ubabaishaji hivyo atamchukulia hatua kali meneja yeyote wa Tarura ambaye
anafanya kazi kwa mazoezi badala ya kushirikisha viongozi wa maeneo husika.
Meneja wa wakala wa barabara nchini
(Tanroads) mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa alisema wanasimamia
mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 1,656 na madaraja 217, kati ya hizo
kilometa 206 ni barabara kuu na kilometa 1,449 ni barabara za mkoa.
Mhandisi Rwesingisa alisema kilometa
206 za barabara kuu ni za lami kufuatia kukamilika kwa kipande cha Bereko-
Bonga kwenye barabara ya Dodoma-Babati.
Alisema kwa upande wa kilometa 1,449
za barabara za mkoa, kilometa 40 ni za lami na kilometa 1,409 ni za changarawe.
"Hali ya barabara ni ya
kuridhisha ingawa kuna baadhi zinapitika kwa shida wakati wa mvua hususani
zilizopandishwa daraja mwaka 2009 kutoka kuwa za wilaya hadi kuwa za
mkoa," alisema mhandisi Rwesingisa.
Alitaja baadhi ya barabara
zilizoathirika na mvua zilizonyesha hivi karibuni ni Mbuyu wa Mjerumani-Mbulu,
Kibaya-Dosidosi, Kilimapunda-Kidarafa, Losinyai-Njoro, Mogitu-Haydom na
Singe-Kimotorok-Sukuro.
Meneja wa Tarura wilaya ya Simanjiro,
mhandisi Martin Mwashambwa alisema wilaya hiyo ina mtandao wa barabara upatao
kilometa 1,373.68
Mhandisi Mwashambwa alisema barabara
za wilaya ni kilometa 932. 58 barabara za vijiji kilometa 327.96 na barabara za
miji ni kilometa 137.14.
No comments:
Post a Comment