Wanachama 3,500 wa Chadema katika
Kijiji cha Narakauwo, Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro, wamejiunga na CCM
kwa lengo la kumuunga mkono Rais John Magufuli na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti.
Wananchi hao ambao awali walikuwa
CCM, waliondoka kwenye chama hicho na kujiunga na Chadema, baada ya kigogo
mmoja kukata majina ya baadhi ya wagombea waliokuwa wanawaunga mkono kwenye
Kijiji hicho na kata hiyo mwaka 2015.
Akizungumza jana wakati akiwapokea
wanachama hao wapya kwenye mkutano uliofanyika kijiji cha Narakauwo, Mnyeti
ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM Mkoani Manyara, alitoa onyo kwa
wanasiasa wanaowayumbisha wananchi wa eneo hilo.
Mnyeti alisema kuna baadhi ya
viongozi wa wilaya hiyo bado wamelala kwani wanadhani huu ni wakati wa kufanya
siasa ili hali ilishakwisha mwaka 2015 na huu ni wakati wa kufanya kazi.
"Kuna baadhi ya viongozi walikaa
vikao usiku ili kukwamisha suala hili, nawapa onyo la mwisho, kama kuna mtu
anataka ubunge asubiri mwaka 2020 siyo leo," alisema Mnyeti.
Hata hivyo, Mnyeti alimuagiza mkuu wa
wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula kuhakikisha anamaliza mgogoro wa uongozi
wa kijiji hicho.
"Mkuu wa wilaya baada ya siku
nne rudi hapa ufanye mkutano wa kijiji kama hawa wajumbe wa serikali ya kijiji
ndiyo tatizo fuateni taratibu zote waondoke uchaguzi ufanyike upya,"
alisema Mnyeti.
Alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri ya wilaya hiyo Yefred Myenzi kuhakikisha uchaguzi mdogo wa kujaza
nafasi za uenyekiti unaofanyia Machi 25, ujumuishe na kijiji hicho.
Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro,
Ally Kidunda alisema eneo hilo halina upinzani ila wanachama hao waliondoka kwa
sababu ya hasira.
Kidunda aliahidi kutoa ushirikiano wa
dhati kwa wanachama hao wapya ili kutimiza dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya.
Mmoja kati ya wanachama hao wapya,
Mathayo Lesenga alisema awali waliondoka CCM baada ya wagombea waliokuwa
wanawaunga mkono kukatwa majina yao.
Lesenga alisema wananchi wa eneo hilo
walikuwa na imani na CCM lakini baada ya kuona kunafanyika ukiritimba walijitoa
na kuhamia Chadema ila sasa hivi wamerudi ili kumuunga mkono Rais Magufuli na
Mnyeti.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,
kata hiyo ilimchagua diwani wa Chadema, Ezekiel Lesenga (Mardadi) na mbunge
James Ole Millya (Chadema) na mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa
aliongoza kwa kura nyingi.
No comments:
Post a Comment