Friday, 16 March 2018

GENDABI KUNUFAIKA NA CHUMVI



Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, kushoto akimsikiliza mzee wa kimila Gidamis Shahanga baada ya kutawazwa kuwa chifu wa jamii ya kidatoga Wilayani Hanang kwenye ziara yake ya siku tano.


Mkazi wa mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang' John Aloyce akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, aliyeahidi kumnunulia bajaji jana itakayomwezesha kutembelea na kumpatia ajira.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akizungumza na wananchi wa Kata ya Gendabi Wilayani Hanang' jana ambapo aliwaahidi kuhakikisha mwekezaji anaanzisha kiwanda cha chumvi kwenye eneo hilo. 


Wananchi wanaozunguka mgodi wa madini ya chumvi ya Gendabi Wilayani Hanang' wanatarajia kunufaika na rasilimali hiyo, baada ya Serikali kupata mwekezaji atakayejenga kiwanda cha chumvi eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza jana kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano wilayani humo alisema atawachukulia hatua kali wanasiasa watakaokwamisha mradi huo. 

Mnyeti alisema wapo baadhi ya wanasiasa wanaotumia matatizo ya wananchi kuwa fursa hivyo hawezi kukubali wakwamishe mradi huo mkubwa wenye faida kwa jamii. 

"Nimesikia hapa kuna baadhi ya wanasiasa wanatumia shida za watu kujinufaisha kisiasa, sasa nikimkuta anapinga hili nitamshughulikia bila kujali chama chake,," alisema Mnyeti. 

Alisema kiwanda hicho kitakapoanza uzalishaji hivyo wananchi wa eneo hilo wajiandae kunufaika kiuchumi kwa kuchimba chumvi kwa wingi na kuuza kiwandani hapo. 

"Haya ndiyo maendeleo tunayosema siyo siasa za maji taka kwani chumvi itakuwa na thamani kubwa tofauti na hivi sasa kwani kiwanda kitawanufaisha," alisema Mnyeti. 

Aliwataka wananchi wa eneo hilo kujiweka tayari na uwekezaji huo ili kuhakikisha uzalishaji unafanyika wa kutosha kwani soko la uhakiki litakuwepo kwa kadiri watakavyofanya uzalishaji. 

"Suala la miundombinu ya barabara watu wa wakala wa barabara za mijini na vijijini (Tarura) wametuhakikishia kufanikisha hilo ili uwekezaji huo usikwame," alisema Mnyeti. 

Mkazi wa eneo hilo Paulo Baso alisema wanakabiliwa na baadhi ya changamoto kwenye machimbo ya chumvi ikiwemo miundombinu na soko la uhakiki la kuuza chumvi hiyo. 

Baso alisema pia vifaa vya kuchimbia chumvi hivyo ni tatizo kwani vyombo vya kutolea chumvi bado ni tatizo ila kupitia kiwanda hicho wanatarajia kuongeza kipato chao. 

Alisema hata bei ya chumvi hiyo inazidi kushuka kutokana na soko kwani debe moja hununuliwa kwa sh1,000 badala ya sh5,000 iliyokuwepo awali. 

Mwenyekiti wa CCM wilayani Hanang, Mathew Darema alisema tatizo la ukosefu wa soko la chumvi linawakabili wachimbaji wengi wanaojishughulisha na shughuli hizo. 

"Tunamshukuru mkuu wetu wa mkoa kwa kufanikisha uwekezaji huu mzuri ambao kwa namna moja au nyingine utanufaisha jamii ya eneo hili kwa kuongeza ajira," alisema Darema. 

No comments:

Post a Comment