Friday 16 March 2018

WANAWAKE WATOA MSAADA KWA WATOTO YATIMA LIGHT IN AFRICA


Mmiliki wa kituo cha watoto yatima na wenye uhitaji maalum, cha Light in Africa cha Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, Lynn Elliott akimpa mkono mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Ester Mahawe, baada ya kupokea msaada wa vyakula na vifaa vya shule.

Mtumishi wa huduma ya Upendo wa Yesu ya Njiro jijini Arusha, Rachel Mmasi akitoa msaada wa shilingi laki tano, kwa ajili ya watoto yatima 69 wa kituo cha Light in Africa cha Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.


Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Ester Mahawe (CCM) na viongozi wa UWT Wilayani Simanjiro, wameshiriki kula chakula cha mchana na kuwapa msaada wa vyakula na vifaa vya shule, watoto yatima 69 wa kituo cha Light in Africa cha Mji mdogo wa Mirerani, kwa lengo la kuwafariji. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Mahawe aliwataka watoto hao wasome kwa bidii na kutokata tamaa sababu ya kukosa wazazi kwani jamii ndiyo wazazi wao waliopo. 

Mahawe alisema jamii inapaswa kuwaunga mkono watoto yatima na wenye uhitaji kwa kuhakikisha wanajitoa kwa hata kidogo walichonacho ili wapate amani mioyoni mwao. 

"Mungu amekupa ulichonacho je wewe umefanyaje kwa hawa yatima, umewavusha hata barabarani ili wasigongwe na gari, umejinyima nini wewe na watoto wako ili yatima wapate?" alihoji. 

Mtumishi wa huduma ya Upendo wa Yesu ya Njiro jijini Arusha, Rachel Mmasi, ambaye aliwapa watoto hao sh500,000 alisema wanatoa huduma ya kiroho kwa watoto wa vituo 12. 

Mmasi alisema wanatoa huduma ya kiroho kwa wanawake, wanaume na watoto, hivyo msaada huo ni miongoni mwa sadaka wanazopokea. 

Mmoja kati ya watoto hao Ester Fred, aliwashukuru wote waliowatembea na kutoa misaada hiyo iliyowapa imani kuwa bado wana wazazi wao. 

Alitoa wito kwa jamii kuiga kitendo hicho, kwani wao ni yatima lakini bado wanahitaji huduma nyingi ikiwemo elimu, chakula na mengineyo.  

Mmiliki wa kituo hicho, Lynn Elliott aliwashukuru wanawake hao kwa kujitolea na kuhakikisha watoto yatima hao na wenye uhitaji maalum wanapata faraja. 

Elliott alisema aliamua kuanzisha kituo cha kulea watoto yatima na wenye uhitaji maalum baada ya kuona baadhi yao wanavyoteseka. 





No comments:

Post a Comment