Wednesday 21 May 2014

TANZANIA KINARA BIASHARA MENO YA TEMBO



Chanzo Mwananchi

Kwa hali ilivyo sasa, inatabiriwa kuwa baada ya miaka saba, kama jitihada hazitafanyika, tembo watatoweka katika ardhi ya Tanzania.
Inakadiriwa kuwa kwa siku, katika mbuga mbalimbali nchini tembo wapatao 30 huuawa kwa ajili ya kupata meno yao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuwalinda Tembo (TEPS), Alfred Kikoti anasema kwa kasi hii, ifikapo mwaka 2020 Tanzania haitakuwa na tembo hata mmoja katika mbuga zake.
Biashara ya pembe za ndovu inaripotiwa kushamiri katika Bara la Afrika, hali inayohatarisha kupotea kwa viumbe hao duniani.
Inaelezwa kuwa ujangili hufanyika kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vikundi vya waasi katika nchi zenye machafuko, kuendesha biashara hiyo na baadhi ya watu waliopewa vibali maalumu vya uwindaji kutumia mwanya huo kufanya ujangili.
Ujangili unaripotiwa kuwa tishio katika sekta ya utalii, kutokana na idadi kubwa ya tembo kuuawa kila mwaka. Sekta hii imekuwa ikichangia kiasi kikubwa katika pato la taifa na wanyamapori pekee wamekuwa kivutio kikubwa cha utalii.
Inakadiriwa kuwa mwaka 2013, uwindaji halali uliingizia Tanzania Dola 50 milioni za Kimarekani ambazo ni wastani wa Sh900 bilioni). Hii inafafanuliwa kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya mapato ya sekta ya utalii yanatokana na wanyamapori.
Kuongezeka kwa kasi ya ujangili nchini kunaelezwa kusababishwa na vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na kuwapo mfumo dhaifu wa usimamizi wa sheria katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ripoti hiyo linayoitwa ‘Ivory’s Curse: The Militarization and Professionalization of Poaching in Africa’, inaeleza kuwa tangu mwaka 2000, wizara hiyo imetawaliwa na kashfa za rushwa mpaka kusababisha zilzosababisha mawaziri na watendaji wakuu kujivua au kuvuliwa nyadhifa zao.
Taasisi ya Kimarekani ya Utunzaji Wanyamapori ya Born Free USA, kwa ushirikiano na Shirika la Ripoti za Kichambuzi na Takwimu la C4ADS, wamefafanua katika ripoti hiyo jinsi vikundi mbalimbali vya waasi barani Afrika wanavyoendesha shughuli za ujangili.
Tanzania inaelezwa kuwa na mfumo mbaya wa usimamizi wa sheria katika kuwasimamia watu wenye vibali vya uwindaji. Pia, wanaangazia jinsi ujangili unavyofanywa kwa ustadi na watu wenye mtandao mkubwa kimataifa wa kuendesha biashara ya pembe za ndovu duniani.
Nchi nyingine zilizotajwa kuathirika zaidi na ujangili barani Afrika ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Cameroon, Msumbiji, Kenya na Zimbabwe.
Hali ya ujangili nchini
Ripoti hiyo inaeleza kuwa idadi ya tembo katika Hifadhi za Selous na Mikumi kwa mwaka 1976, ilikuwa ni 109,419, lakini mwaka 2009, idadi hiyo ilishuka mpaka kufikia tembo 38,975.
Utafiti uliofanywa na taasisi ya Frankfurt Zoological Society mwishoni mwa mwaka 2013, inaeleza kuwa ni tembo 13,084 wanaokadiriwa kubakia katika hifadhi hizo, sawa na upungufu wa asilimia 66 katika kipindi cha miaka minne.
Hii imefafanuliwa kuwa zaidi ya tembo 25,000 waliuawa katika hifadhi ya Selous ndani ya miaka minne pekee. Pia inabainisha upungufu wa tembo katika Hifadhi ya Ruaha-Rungwa kutoka tembo 35,461 mpaka tembo 20,090 sawa na upungufu wa asilimia 36.5 kuanzia mwaka 1990 mpaka sasa.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi huu nchini Kenya, inaitaja Tanzania kama kitovu cha usafirisha wa pembe za ndovu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Bandari ya Dar es Salaam inaongoza ikifuatiwa na Mombasa.
Kutoka mwaka 2008 mpaka 2013, inaelezwa zaidi ya tani 20 za pembe za ndovu zilikamatwa zikisafirishwa au kuingizwa katika Jiji la Dar es Salaam. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya C4ADS iliyokuwa ikiripoti juu ya pembe za ndovu zilizokamatwa, Dar es Salaam kuwa ya pili baada ya Mombasa.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa uchunguzi wa vinasaba (DNA) ulifanywa katika tani 11 za pembe za ndovu zilizokamatwa Taiwan, Japan na Hong Kong mwaka 2006, ilibainika kuwa pembe 1500 zilitoka Tanzania katika Mbuga ya Selous.
Uchunguzi huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe hizo vilifanana, hali iliyoleta hisia kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiwinda katika hifadhi hiyo mara kwa mara katika utaratibu maalumu unaotambuliwa na Serikali.
Ripoti inaonyesha kuwa kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi wa uwindaji halali, kwani wawindaji wenye vibali hawasimamiwi ipasavyo kufanya taratibu zilizowekwa kisheria, hali inayowafanya kutumia nafasi hiyo kufanya vitendo vya ujangili.
Kuhusu vitalu vya uwindaji, ripoti inaonyesha kuwa zoezi la utoaji vibali limekuwa likifanyika kwa usiri mkubwa, jambo linalodhaniwa kutoa nafasi ya rushwa katika uwindaji huo. Pia taasisi za kusimamia sheria zinatajwa kutokuwa na njia madhubuti za kusimamia zoezi hilo, jambo inayolirudisha nyuma taifa.
Tuhuma za rushwa wizarani
Ripoti hiyo inawataja baadhi ya waliokuwa mawaziri na wakurugenzi mbalimbali wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuhusika katika kulisababishia taifa hasara kubwa na kushindwa kusimamia kikamilifu udhibiti wa vitendo vya ujangili nchini.
Ripoti inasema wakurugenzi watatu kati ya watano waliokuwapo Wizara ya Maliasili, ikiwajumuisha Wakurugenzi wa Wanyamapori na Misitu, ama waliondolewa kazini au kushushwa vyeo kutokana na utendaji mbaya katika idara zao.
Inaeleza kuwa wizara ilijawa kashfa za rushwa, hali iliyosababisha Norway kuacha kutoa msaada katika Mpango wa Mabadiliko ya Tabia ya Nchi. Ilibainika kuwa kulikuwa na ubadhirifu wa mabilioni ya fedha za mpango huo.
Mwaka jana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili ilifichua ‘madudu’ yaliyofanywa na watendaji waliotumwa kuwakamata watuhumiwa wa ujangili nchini.
Vitendo viovu vilivyofanywa na watendaji hao, vinatajwa kuwa kikwazo katika vita hiyo kwani vilisababisha Serikali kusitisha zoezi hilo hali ambayo inatajwa kuchangia ongezeko la vitendo vya ujangili nchini.
Idara ya Wanyamapori yazungumza
Akizungumzia udhaifu katika usimamizi wa wawindaji halali, kaimu mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Paul Sarakikya alisema siyo kweli kwamba wawindaji halali huachwa bila usimamizi wowote, kwa sababu wana mifumo ya kusimamia zoezi hilo.
Sarakikya alisema idadi ya tembo inazidi kuongezeka katika hifadhi nchini, tofauti na upungufu unaoelezwa katika ripoti hiyo.
“Sikubaliani na ripoti hiyo, tumeshaongea sana juu ya suala hili. Rais (Jakaya Kikwete) alishalizungumzia na waziri pia alishaliongelea. Ufafanuzi ndio huo, hamna ukweli wowote katika ripoti hiyo,” alisisitiza Sarakikya.
Mkurugenzi huyo alihoji kuwa kama hakuna usimamizi madhubuti katika uwindaji halali, wamewezaje kusimamia zoezi hilo miaka yote mpaka idadi ya tembo inaongezeka tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma?
Juhudi zinazofanywa na Serikali
Taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Bunge la Bajeti la 2013/14 ilisema imeimarisha ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori na imefanikisha kuwakamata watuhumiwa 1,215, bunduki 85 na risasi 215 mwaka 2013.
Ilisema kesi 670 zimefunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini kati ya hizo, 272 zimekwisha baada ya washtakiwa 247 kulipa faini ya jumla ya Sh175 milioni na washtakiwa 71 kupewa adhabu ya vifungo vya jumla ya miezi 1,192.
Kati ya hizo, kesi 398 zenye jumla ya washitakiwa 897 bado zinaendelea katika mahakama mbalimbali nchini. Pia Serikali ilikamata nyara zenye thamani ya Sh 855.1 milioni.

No comments:

Post a Comment