Ofisa Polisi Jamii wa Tarafa ya Moipo Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara,
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Amiri Mlemba, akizungumza mwishoni mwa wiki na
wakazi wa Kitongoji cha Kilimahewa Kata ya Endiamtu kuhusiana na suala zima la
polisi jamii na ulinzi shirikishi.
Jamii
Nchini imetakiwa kutoa ushirikiano kwenye suala zima la ulinzi shirikishi na
polisi jamii ili kufanikisha ulinzi na usalama katika maeneo wanayoishi na
kutokomeza ualifu.
Wito
huo umetolewa na Ofisa polisi jamii wa Tarafa ya Moipo Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara, Mkaguzi Msaidizi wa polisi Amiri Mlemba wakati akizungumza na
wakazi wa Kitongoji cha Kilimahewa Kata ya Endiamtu.
Mlemba
alisema jamii ikitoa ushirikiano kwa polisi kupitia dhana ya ulinzi shirikishi
na polisi jamii, uhalifu nchini utapungua na pia wananchi wataishi kwa amani ya
kutosha na kufanya kazi zao za uzalishaji mali bila tatizo lolote.
“Kama
mnavyotambua sisi polisi hatuwezi kufahamu kila jambo na pia wahalifu mnaishi
nao mitaani hivyo kupitia dhana ya polisi jamii na ulinzi shirikishi
tujulisheni wahalifu walipo au sehemu uhalifu unapofanyika ili tuutokomeze,”
alisema Mlemba.
Hata
hivyo, aliwataka wakazi hao kutokuwa na hofu pindi wanapotoa taarifa kwao na
endapo watakuwa na wasiwasi watoe taarifa za uhalifu kwake au kwa mkuu wa kituo
cha polisi Mirerani, SP Ally Mohamed Mkalipa.
Kwa
upande wao, wakazi hao walitoa pongezi kwa askari wa kituo hicho kwa kuwapa
ushirikiano pindi wanapopewa taarifa za uhalifu, hivyo kusababisha ualifu
kupungua kwenye mji mdogo wa Mirerani.
Walidai
kuwa japokuwa askari polisi wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa nyumba za
kuishi hivyo wanapopewa taarifa hutoka nyumbani na kwenda kituo cha polisi kisha
kwenye tukio, lakini wanajitahidi kutimiza wajibu wao.
No comments:
Post a Comment