Friday 11 April 2014

DIWANI LUCAS ZACHARIA AWACHANGI AWANANCHI WAKE CHF


Diwani wa Kata ya Endiamtu, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Zacharia akiwahamasisha wakati wa kitongoji cha Kilimahewa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF), hata hivyo diwani huyo amechangia sh500,000 za kaya 50 kwenye vitongoji vitano vya kata hiyo.


Ili kuwahamasisha wananchi wajiunge na mfuko wa afya ya jamii (CHF) Diwani wa Kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Zacharia amelipia sh500,000 za gharama za matibabu, kwa kaya 50 za watu 300 wa Vitongoji vya Sekondari, Kilimahewa, Endiamtu, Kairo na Zaire vya kata hiyo.  

Akizungumza juzi kwenye mkutano wa kitongoji cha Kilimahewa kilichopo katika kata hiyo, Zacharia alisema wananchi wengi wakijiunga na CHF, dawa na vifaa tiba vitapatikana kwa wingi kwenye kituo cha afya Mirerani. 

Alisema kaya moja yenye baba, mama na watoto wanne wakichangia sh10,000 wanatibiwa kwa mwaka mmoja katika zahanati, kituo cha afya na hospitali kwenye wilaya husika hivyo jamii inatakiwa ichangamkie fursa hiyo. 

“Ndugu zangu, maendeleo yetu Endiamtu kwa pamoja tunaweza, hivyo tujiunge kwa wingi kwenye mfuko huu ambapo watu wengi tukijiunga Serikali inatuunga mkono nusu kwa nusu na kuboresha kituo chetu cha afya,” alisema Zacharia.

Alisema endapo wananchi wakiweza kuchangia sh5 milioni kwenye mfuko huo, Serikali nayo inachangia sh5 milioni na wakichangia sh10 milioni, Serikali pia itachangia kiasi kama hicho hivyo mpango huo una manufaa makubwa. 

Hata hivyo, ili kumuunga mkono Diwani huyo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kilimahewa, Joseph Masasi naye alijitolea sh100,000 kwa kaya 10 zenye baba, mama na watoto wanne wa kila kaya wa kitongoji hicho, watakaotibiwa na mfuko wa CHF.

“Tunashukuru sana na tunampongeza diwani wetu Zacharia, ambaye ni mtu wa watu kwani kwa roho moja amejitolea sh500,000 kwa ajili ya kuwalipia watu wasio na uwezo wakiwemo wajane na yatima,” alisema Masasi.



No comments:

Post a Comment