Sunday 13 April 2014

GURUMO HATUNAYE TENA


"Wanangu wote njooni kaeni chini niwaambie maisha ya sasa ni magumu tofauti na ya zamani, eheeee, eheehe, wakati wa ujana wangu mimi baba yenu mimi baba yenuu, shati dukani shilingi sita unapata na hivi sasa shilingi sita hata soda haupati, na hivi sasa shilingi sita hata mkate hupati eheehee!"

Huo ni wimbo uitwao Wosia kwa watoto, miongoni kati ya nyimbo zilizotungwa na Marehemu Muhidin Maalim Gurumo.

Mkongwe huyu wa muziki nchini aliiaga dunia jana mchana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, ambako alikuwa amelazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia yake, Gurumo alipelekwa kwenye hospitali hiyo juzi baada ya kupatwa na shinikizo la damu.

Taarifa za kifo cha Gurumo zilianza kusambaa kwenye mitandao na ujumbe wa simu za mkononi kama moto uwakao nyikani. Wapo walioziamini, lakini wengine walidhani ni uzushi uliozoeleka katika siku za hivi karibuni, hasa kwa wasanii na watu maarufu.

Binafsi nilipopata taarifa hizo nilishtuka. Ni baada ya kuzungumza na baadhi ya wanamuziki wa bendi yake ya Msondo Ngoma, akiwemo msemaji wa bendi hiyo, Super Deo ndipo nilipoanza kuamini.

Ni kweli kwamba kifo huua mwili wa binadamu ukabaki kuwa vumbi kaburini, lakini yote aliyoyafanya hapa duniani, yatabaki kuwa kumbukumbu ya milele kwa vizazi vya sasa na vitakavyokuja baadaye.

Marehemu Gurumo alitangaza kustaafu kazi ya muziki mwaka jana baada ya kuifanya kazi hiyo kwa miaka 53.

Gurumo (74), alitangaza uamuzi wake huo Agosti 22, mwaka jana alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), mjini Dar es Salaam.

Mkongwe huyo wa muziki alisema aliamua kustaafu kutokana na umri wake mkubwa.

Licha ya kujihusisha na muziki katika sehemu kubwa ya maisha yake, Gurumo alisema hakupata mafanikio makubwa kimaisha, licha ya kujenga nyumba anayoishi na familia yake, iliyoko Ubungo Makuburi, Dar es Salaam.

Katika kipindi alichopiga muziki katika bendi za NUTA, JUWATA, OTTU na Mlimani Park, Gurumo alitunga nyimbo zaidi ya 200.

Alijiunga na NUTA 1964 akiwa mmoja wa waanzilishi kabla ya kuhamia Mlimani Park 1978 na Orchestra Safari Sound (OSS) kuanzia 1985 hadi 1990.

Marehemu Gurumo alikuwa kipaji cha kutunga nyimbo zenye ujumbe kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Alikuwa gwiji katika uimbaji na jina la Gurumo halikuwa la utani kwa sababu ya kuimba kwa sauti nzito, bali ni jina lake halisi.

Aliposimama jukwaani kuimba katika bendi za Msondo Ngoma, OSS na Mlimani Park Orchestra, mashabiki waliburudika kutokana na sauti yake nzito, ambayo ilikolezwa na nyingine za Hassan Bitchuka, marehemu Moshi William, Thobias Chidumule, hayati Hamisi Juma na Maxi Bushoke.

Katika wimbo wa Kassim aliouimba akiwa Mlimani Park, Gurumo akishirikiana na Hamisi Juma (sasa marehemu), aliimba na kutoa picha halisi ya mlevi wa pombe aliyeanza kufilisika na kubana matumizi, wakati Hamisi aliimba kama mwanamke, aliyezoea kupewa ofa na Gurumo.

“Na mie moja Kassim,” anaimba Hamisi katika wimbo huo.

“Sina hela ya mchezo,” anajibu Gurumo.

Wimbo mwingine uliompa sifa Gurumo ni Celina aliouimba akiwa na Mlimani Park. Katika wimbo huo, Gurumo anasikika akiimba: ‘Na kwa sababu imekuwa hivyo Celina, sioni haja ya kutaka ujiue kwa ajili yangu”. Wimbo huo ulitungwa na marehemu Joseph Mulenga, aliyekuwa akipiga gitaa la solo.

Akiwa OSS, alipata umaarufu kupitia wimbo wa Chatu mkali. Katika wimbo huo, sauti yake nzito inasikika alipoimba: ‘Natoa onyo kwa yeyote anayemchezea chatu ni hatari, atakuwa asipate lolote la manufaa, na ajali imkute bila ya kutegemea, atakuja adhirika ajute na dunia.

Nyimbo zingine, ambazo zinakumbusha kazi ya Gurumo tangu alipojitosa kwenye fani ya muziki ni ‘Salima’, ‘Bwana Abdul’, ‘Dada Fatuma’, ‘Kulima Hadeka’ (umelima bondeni) na ‘Agweti Chole’ (Mwenzangu Twende) zilizoimbwa kwa lugha ya Kizaramo. Alitunga nyimbo hizo alipokuwa Kilwa Jazz.

Gurumo alizaliwa 1940 katika kijiji cha Masaki, Kisarawe mkoani Pwani. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Sungwi na kumaliza darasa la saba 1956. Pia alipata mafunzo ya dini ya Kiislamu katika madrasa ya kijiji alichokuwa akiishi.

Baada ya kumaliza shule, aliamua kujiunga na bendi ya Kilimanjaro Chacha iliyokuwa na maskani Ilala, Dar es Salaam. Alifanya kazi na bendi hiyo hadi 1961 alipojiunga na Rufiji Jazz pia ya Dar es Salaam.

Alidumu na bendi hiyo hadi 1963 alipojiunga na Kilwa Jazz, iliyokuwa maarufu enzi hizo chini ya uongozi wa marehemu Ahmed Kipande. Bendi hiyo ilikuwa na makundi mawili, Kilwa A na B, Gurumo alikuwa kundi B.

Gurumo hakupendezwa na uamuzi wa marehemu Kipande kumuweka katika kundi B, wakati alijiona ana uwezo mkubwa wa kuimba kuliko baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi A. Hali hiyo ilimfanya ajiunge na NUTA Jazz 1964.

Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Jumuia ya Wafanyakazi Tanzania na baadaye ilibadili majina na kuitwa JUWATA na OTTU Jazz. Baada ya jumuia hiyo kujitoa katika kuendesha bendi, ilikabidhi vyombo kwa wanamuziki, ambao waliamua kuibadili jina na kuiita Msondo Ngoma.

Akiwa OTTU hadi Msondo Ngoma, alitunga nyimbo nyingi ukiwemo wa ‘Wosia kwa Watoto’.

Gurumo ndiye muasisi wa mitindo ya muziki ya Msondo, akiwa na NUTA, JUWATA na OTTU Jazz, Sikinde akiwa na Mlimani Park na Ndekule akiwa na OSS, ambayo ilizipatia umaarufu mkubwa bendi hizo.

Mitindo hiyo ya muziki ilitokana na majina ya baadhi ya ngoma za kabila la Wazaramo na huchezwa kama ilivyo ngoma ya Vanga.

Tofauti ni kwamba, wachezaji wa ngoma hizo huvaa mavazi ya asili, wakati wale wa muziki wa dansi huvaa mavazi ya kawaida.

Kabla ya uamuzi wa kustaafu muziki, Gurumo alishauriwa na daktari aliyekuwa akimtibu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, kujiweka kando na masuala ya muziki baada ya kuugua ugonjwa wa moyo na kulazwa hospitali mara kadhaa.

Ugonjwa wa moyo hutokana na kupungua damu inayoingia kwenye mishipa ya moyo, ambao haukumpata Gurumo kwa sababu ya kuimba.

“Sijapatwa na ugonjwa huu kwa sababu ya kuimba kwa miaka mingi. Baada ya kupata tiba, madaktari walinishauri nipumzike kwa sababu ya umri kubwa mkubwa, siwezi tena kusimama jukwaani kwa muda mrefu na kuimba,” anasema. Alianza kusumbuliwa na maradhi mwaka 2011.

Gurumo ni mmoja wa wanahisa wa bendi ya Msondo. Wengine ni Saidi Mabela, Saidi Kibiriti (meneja), Ramadhani Zahoro, Abdul Ridhiwani, Roman Mng'ande na Huruka Uvuruge.

Wanamuziki hao wanamiliki kiwango sawa cha hisa na malipo yao kwa mwezi ni makubwa ikilinganishwa na waajiriwa.


No comments:

Post a Comment