Sunday, 27 April 2014

MAHAFALI YA SHULE YA SEKONDARI DR OLSEN



Wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne wametakiwa wasiridhike na elimu waliyoipata hivyo wajiendeleze zaidi kwenye vyuo mbalimbali kwa manufaa yao ya baadaye kwani kuhitimu elimu hiyo siyo mwisho wa kusoma.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Ofisa Elimu wa mkoa wa Manyara, Ibrahim Mbang’o kwenye mahafali ya tano ya kidato cha sita kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Dr Olsen iliyopo Wilayani Mbulu.
Mbang’o alisema hatua waliyofikia ni mwandelezo wa safari ya taaluma hivyo kuhitimu siyo mwisho wa elimu ila wanatakiwa kupiga hatua nyingine na kuhakikisha wanafaulu mitihano yao na kuingia chuo kikuu.
“Hatua mliyofikia ni kubwa hivyo jiendelezeni zaidi na msikubali kuolewa au kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na ulevi jamani someni na kufikia hatua ya juu zaidi” alisema Mbang’o.
Alisema watumie elimu waliyoipata kwa kujiendeleza zaidi na aliwapongeza kwa kufikia hatua hiyo kwani walijilisha na kujiepusha na tamaa na kutawala nafsi zao, vishawishi na anasa nyingine.



 Mwanafunzi wa kidato cha sita wa shule hiyo, Jackline Nanyaro akionyesha namna ya kumpasua panya kwenye somo la baiolojia katika mahafali ya sita ya shule hiyo.
Naye, mkuu wa shule ya Dr Olsen, Ernest Asseri alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1997 ikiwa na kidato cha kwanza na mwaka 2007 ilianzishwa kidato cha tano na sita kwenye michepuo ya PCB na CBG.
Asseri alisema hadi hivi sasa wana wanafunzi 22 wa kidato cha sita wanaotarajia kufanya mtihani wa kidato cha sita May 5 mwaka huu na wanatarajia kufaulisha wanafunzi wengi kwenda vyuo vikuu.
Alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mdondoko na utoro kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne, upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati kwa kidato cha tano na sita.   

No comments:

Post a Comment