Thursday 17 August 2017

WAHADZABE WALIA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA WADAI WANAKOSA ASALI NA MATUNDA

 Jamii ya warina asali, waokota matunda, wawindaji wa kihadzabe wa Kijiji cha Domanga Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, wamewalalamikia wakulima na wafugaji walioingia kwenye bonde la Yaeda Chini, kuwa wanawaharibia mazingira na kusababisha wakose asali na matunda.

Wahadzabe hao walitoa kilio chao baada ya Mkuu wa wilaya hiyo, Chelestino Mofuga kutembelea kwenye kijiji hicho kilichopo kata ya Eshkesh na kuzungumza nao masuala mbalimbali ya maendeleo.

Mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo, Gendo Gutanai alisema wanakabiliwa na wakati mgumu hivi sasa, kutokana na mazingira yao kuharibiwa na wakulima na wafugaji hao.

Gutanai alisema wao kama jamii ya wahadzabe hawajishughulishi na kilimo au ufugaji kwenye bonde hilo ila shughuli za kilimo na ufugaji zinazofanyika zinaharibu mazingira ya eneo hilo.

 "Sisi hatuna shughuli nyingine mbadala zaidi ya kurina asali, kuokota matunda hasa mibuyu na kuwinda baadhi ya wanyamapori, lakini hawa wakulima na wafugaji wanatuharibia mazingira yetu," alisema.

Alisema pia wanaomba kupatiwa nafasi ya kuwashirikisha katika ngazi ya maamuzi mbalimbali ya kata na ya wilaya, ili na jamii hiyo wawe na watetezi wao kwenye masuala tofauti.

"Na sisi tunataka tuwe na wawakilishi wetu kwenye ngazi ya udiwani na ubunge ili waweze kutusemea juu ya changamoto mbalimbali zinazotukabili katika eneo hili," alisema.

Hata hivyo, mkuu wa wilaya hiyo, Chelestino Mofuga alimuagiza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hudson Kamoga, kutuma wataalamu kusimamia mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kulinda mazingira hayo.

"Pamoja na hayo halmashauri ya wilaya iwasogezee huduma ya maji na afya kwenye kata ya Eshkesh ili kunusuru maisha yao," alisema Mofuga.

Aliwataka wananchi wa jamii hiyo kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uwakilishi ili waweze kupata viongozi wa kuwasemea ikiwemo hivi sasa wagombee nafasi kupitia CCM inayofanya uchaguzi kwenye nafasi tofauti.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Hudson Kamoga alisema wameshatenga sh40 milioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Eshkesh.

Mtafiti aliyeishi na wahadzabe kwa zaidi ya miaka 20, Daud Beroff alisema ameandika kitabu cha historia ya wahadzabe ambacho kitauzwa na fedha zitakazopatikana zitatumika kusomesha watoto wa jamii hiyo.


No comments:

Post a Comment