Thursday, 17 August 2017

VURUGU ZAZUIA UCHAGUZI WA CCM KATA YA ENDIAMTU MJI MDOGO WA MIRERANI

  
KATIKA hali ya kushangaza, vurugu kubwa zimezuka kwenye uchaguzi wa viongozi wa CCM Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, baada ya baadhi ya wanachama kupinga majina ya wagombea wanaowaunga mkono kukatwa.

Kutokana na vurugu hizo, mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, Mratibu Msaidizi wa polisi (ASP) Evarest Makala, akiwa na askari polisi walifika mara moja kwenye uchaguzi huo na kuagiza usitishwe mara moja kutokana na hali ya usalama kutokuwa nzuri.

Chanzo cha vurugu hizo zilizotokea kwenye uchaguzi huo ni kukatwa majina ya wagombea wanaoungwa mkono na wanachama wengi na kupitishwa majina ambayo yanadaiwa kuwa ni watu dhaifu wasioweza kukivusha salama chama hicho kilichopoteza nafasi ya udiwani na ubunge kwa wapinzani wao wa Chadema.

Hali ya hewa ilianza kuchafuka baada ya wasimamizi wa uchaguzi huo, Mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM wilaya hiyo Awadhi Omari na Katibu wa UVCCM wa wilaya hiyo Bakari Mwacha kusoma majina ya waliopitishwa kugombea nafasi mbalimbali.

Mwacha alitaja majina matatu yaliyopitishwa kugombea uenyekiti wa CCM wa kata hiyo ni Claudia Dengesi, Paul Kiula na Sifael Saitore na kuzusha sintofahamu baada ya kukosekana kwa mgombea Elisha Mnyawi, ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite.  
 Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tupendane, Isaya Abayo alihoji sababu ya jina la Claudia Dengesi kurudishwa kugombea uenyekiti wa kata hiyo, ili hali alishachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa jumuiya ya UWT ya kata hiyo na kukata majina ya wagombea wengine wenye uwezo mkubwa wa kiutendaji.

"Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alishatoa maagizo kuwa kwenye CCM mpya ni mtu mmoja na nafasi moja, sasa itakuwaje huyu mama anapatiwa nafasi nyingine ya kugombea wakati ni Mwenyekiti wa UWT," alisema Abayo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tanesco, Justin Abraham alisema CCM ni chama cha wanachama wote na kila mwanachana ana hisa moja, hivyo chama hicho kisigeuzwe kuwa kundi la familia kwani kila mwanachama ana haki ya kugombea.

"Mimi sina imani na hawa wasimamizi kwani ndiyo wanasababisha migogoro kwenye hizi kata za Mirerani na Endiamtu, badala tuungane ili kuwaondoa Chadema kwenye kata na wilaya ," alisema Abraham.
Mwanachama mwingine Japhary Matimbwa alisema ni jambo la kushangaza kwa kukatwa majina ya watu makini wenye ushawishi mkubwa kwa jamii na viongozi, huku majina ya watu dhaifu na mengine ya familia moja kupitishwa kwa upendeleo.

"Haiwezekani jina la meya wa mji mdogo wa Mirerani Adam Kobelo na mtu makini kama Elisha Mnyawi na Oscar Gunewe yanakatwa, kisha yanapitishwa mengine ambayo hayana ushawishi kwa jamii, hawa hawawezi kukipitisha chama kwenye huu wakati mgumu," alisema Matimbwa.

Hata hivyo, mmoja kati ya wasimamizi hao Bakari Mwacha aliwaambia wanachama hao kuwa, wenyewe ni wasimamizi tuu wa uchaguzi huo na suala kupitishwa majina, linahusu ngazi ya viongozi wa CCM wa wilaya na mkoa.

Kutokatana na majibu hayo kukaanza kutokea vurugu zilizosababisha askari polisi wa kituo cha Mirerani wakiongozwa na mkuu wa kituo hicho ASP Makala kufika mara moja na baada ya kusikiliza maelezo ya viongozi hao na wanachama aliagiza uchaguzi huo usitishwe kufanyika, kutokana na hali ya usalama kuwa ndogo.


No comments:

Post a Comment