Pili Hussein ni mmoja katiya wanawake wachache wa Mji
mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, waliobahatika kuwa na
mgodi wa madini ya Tanzanite.
Akiwa mmiliki wa mgodi huo, Pili alibahatika kupata madini ya
Tanzanite na kufanikiwa kuwekeza kwenye miradi mbalimbali na kujenga nyumba,
kununua magari, mashamba, matrekta na pikipiki.
Kuchimba
madini ni kazi ngumu ya shuruba yenye kuhitaji mitulinga, yeye ni
mwanamke alifanikiwa kwa namna ipi kuzamia mgodini na kufanya kazi hiyo
bila kugundulika kuwa ni mwanamke.
Pili Hussein ambaye
anaelezea changamoto alizozipata mara baada ya kufika kwa mara ya kwanza miaka
ya 80 kwenye machimbo hayo ya Tanzanite
Mwandishi:Ilikuaje ulipofika kwa mara ya kwanza kwenye machimbo ya
madini ya Tanzanite?
Pili: Wanawake walikuwa hawaruhusiwi kuzamia mgodini hivyo
nikatamani kufanya shughuli hiyo ya kuchimba madini ili nipate fedha nyingi
hivyo ilinibidi nibadili jina na kujiita mjomba Hussein kasha nikakata suruali
zangu zikawa kaptula nikawa nazivaa na kuzamia mgodini.
Mwandishi: Baada ya hapo ikawaje?
Pili: Nilikuwa kama mwanaume kabisa kwani nilifunga panga kiunoni
nikizamia mgodini umbali wa zaidi ya mita 100 chini ya ardhi kwenye vumbi, joto
huku nikifanya kazi hiyo ngumu kama mwanaume halisi kumbe mimi ni mwanamke.
Mwandishi: Ulifanikiwa kupata madini ya Tanzanite ulipokuwa
unachimba madini hayo?
Pili: Baada ya muda wa mwaka mmoja na miezi kadhaa nilipata
utajiri wa madini hayo ya Tanzanite, kisha nikawajengea nyumba wazazi wangu
mkoani Singida, ndugu zangu pia nikawajengea nyumba kisha nikaanzisha mgodi
wangu binafsi ambao nao ulikuja kutoa madini nikanunua mashamba, magari, trekta,
pikipiki na kujenga nyumba.
Mwandishi: Katika uchimbaji wako migodini, wachimbaji hawakuwahi
kukuhisi kama wewe ni mwanamke?
Pili: Haikuwahi kutokea hivyo kwani hata sauti yangu ilikuwa ni
kubwa ila siku moja ilitokea mwanamke alibakwa na watu kadhaa na polisi walipokuja
kutukamata ndipo nikaeleza ukweli mtupu kwa kufika kituoni na kuwaomba askari
wa kike wanikague kama nina uwezo wa kubaka na waliponiangalia ndipo wakabaini
kuwa mimi ni mwanamke japo watu hawakuamini ila baadhi hawakuamini hadi nilipoolewa
mwaka 1991 ndipo wakaamini.
Mwandishi:Kuna wanawake ambao wanazamia mgodini hadi hivi sasa?
Pili: Zaidi yangu mimi hakuna mwanamke ambaye anazamia mgodini
kama mimi ila wapo wapishi migodini na ambao wanachekecha mchanga au udongo
uliotoka mgodini ambao wanafanya shughuli hiyo juu mgodini ila hawaruhusiwi
kuingia mgodini.
Mwandishi: Unatoa wito gani kwa Serikali kuhusiana na kuwajengea
uwezo wanawake wanaomiliki migodi, ambao wanachimba madini ya Tanzanite?
Pili: Serikali inapaswa kuwapa kipaumbele wanawake wanaomiliki
migodi na kuchimba madini ya Tanzanite kwa kuwapatia mikopo kwani wengi wao wanakabiliwa
na changamoto kubwa ya ukosefu wa fedha za uendeshaji wa shughuli za migodini
hasa sisi ambao migodi yetu haijatoa madini kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment