Tuesday 1 August 2017

DC AZINDUA KAMPENI YA KUPIMA UJAUZITO

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amezindua kampeni ya kuwapima ujauzito wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Wilayani humo kwa lengo la kupiga vita watoto wa kike kupata mimba mashuleni.  

Akizungumza wakati kuzindua zoezi hilo, Mofuga alisema kauli mbiu ya Mbulu bila mimba za wanafunzi na tuache watoto wa kike wasome inapaswa kutekelezwa kwa vitendo. 

Alitoa agizo kwa mkurugenzi wa mji wa Mbulu Anna Mbogo, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga na maofisa elimu kuhakikisha wanaendesha zoezi la upimaji mimba kila baada ya miezi mitatu. 

Alisema huo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa hivi karibuni ili kuhakikisha hakuna wanafunzi wajawazito na waliozaa watakaoendelea na masomo katika mfumo wa kawaida.  

"Natoa onyo kwa baadhi ya walimu na wananchi makatili wanaojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi kwani watapata adhabu kali ya kwenda jela miaka 30 na kazi ngumu kwani hili limeshazungumzwa na Rais Magufuli," alisema Mofuga.

Aliwataka wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu wa shule za msingi kusimamia taaluma na nidhamu na kuwafichua wazazi na walezi wanaoficha wahalifu wanaowapa mimba wanafunzi na wanaokubali kuwaozesha. 

"Rais Magufuli alishatoa agizo kuwa sasa hivi wanafunzi wasome bure, hivyo badala ya kutumia fursa hiyo wazazi na walezi wanawaozesha wasichana au kuwachungisha mifugo wavulana, hao wote nitawachukulia hatua kali," alisema Mofuga. 

Mmoja kati ya wakazi wa mji wa Mbulu, Yohana Amnaay alisema jamii inapaswa kuunga mkono zaidi juhudi zilizoonyeshwa na mkuu huyo wa wilaya ili wanafunzi wa kike wapate elimu bora. 

"Suala la kwenda kwa mazoea hivi sasa limekwishwa kwani tumeona juhudi za mkuu wa wilaya kupiga vita watoto wa kike kupata mimba na kuwachukulia hatua wanaowapa mimba wanafunzi," alisema Amnaay. 


No comments:

Post a Comment