Wednesday 23 August 2017

SIMBACHAWENE AIMWAGIA SIFA SIMANJIRO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene amezitaka wilaya nyingine kuiga wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara kwa namna ilivyojenga majengo ya madarasa, maabara na nyumba za walimu kwa ubora na thamani ya fedha zilizotengwa. 

Waziri Mkuchika akizungumza kwenye ziara yake ya siku moja Wilayani Simanjiro alipitia katika shule ya sekondari Loiborsiret Wilayani Simanjiro alisema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwani majengo yamesimamiwa vizuri na kujengwa kwa ubora unaotakiwa. 

Alisema viongozi wa wilaya nyingine nchini wanapaswa kupata somo kupitia ujenzi huo ambao thamani ya fedha inaendana na thamani ya ujenzi wa miundombinu iliyofanyika kwenye shule hiyo ya sekondari. 

Alisema baadhi ya maeneo unakuta viongozi wanashindwa kusimamia vyema na kujenga majengo ya shule yenye ubora, ambayo baada ya muda mfupi yanaweka nyufa na yanabomoka. 

"Pamoja na hayo nawapongeza pia wanafunzi wa shule hii ambao wengi wao ni jamii ya kifugaji wa kimasai ambao baadhi yao nimekagua madaftari yao na kubaini kuwa kiwango cha taaluma ni kizuri tofauti na matarajio yangu, hongereni sana walimu wa shule hii," alisema Simbachawene. 

Alisema walimu wa shule hiyo wanastahili pongezi nyingi kwa kufanya kazi yao kwa uadilifu na pia wanafunzi nao kwa upande wao wanafunzi wanatimiza wajibu wao kwa kusoma ipasavyo. 

Mhandisi wa ujenzi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Martin Mwashambwa alisema ujenzi huo umegharimu kiasi cha sh219.9 milioni, pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT). 

Mhandisi Mwashambwa alisema ujenzi huo umehusisha nyumba kubwa yenye uwezo wa kuishi familia sita iliyogharimu sh149.9 milioni na vyumba viwili vya madarasa vya thamani ya sh49.6 milioni. 

Mhandisi huyo alitaja ujenzi mwingine ni vyoo vya wanafunzi wa shule hiyo uliohusisha matundu nane yenye thamani ya sh20. 3 milioni. 

Mkuu wa wilaya hiyo, mhandisi Zephania Chaula alimshukuru Waziri Simbachawene kwa pongezi hizo alizozitoa kwao kutokana na ubora wa ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo ya sekondari Loiborsiret. 

"Mheshimiwa Waziri, ukiwa na mkuu wetu wa mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera, nakuhakikishia kuwa hatutalala usingizi na kubweteka kwa sifa hizo ila tutaongeza juhudi zaidi juu ya ujenzi bora wa majengo ya serikali," alisema mhandisi Chaula. 

No comments:

Post a Comment