Wednesday 23 August 2017

SIMBACHAWENE AINGILIA KATI MGOGORO SIMANJIRO

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene ameingilia kati mgogoro wa muda mrefu wa kugombea kitongoji cha Katikati, baina ya vijiji viwili vya Sukuro na Kitiangare, vilivyopo kata ya Komolo, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Waziri Simbachawene amewapa ahadi ya muda wa wiki mbili, wananchi wa kata hiyo kuwa atamaliza mgogoro huo unasababisha migongano ya jamii ya eneo hilo, ambao kwa muda mrefu wengi wao wanaishi kwa kubaguana. 

Hadi hivi sasa kitongoji hicho hakina uongozi kutokana na mgogoro huo wa muda mrefu uliosababisha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Christopher Ole Sendeka (mkuu wa mkoa wa Njombe) na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Manyara, Henry Sheriff (Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga) kulumbana kwenye mkutano wa ndani. 

Waziri Simbachawene akizungumza kwenye mkutano wake na wananchi wa kata hiyo uliofanyika katika kijiji cha Sukuro, alisema baada ya muda huo mgogoro huo utamalizika ili ijulikane kitongoji hicho kitapelekwa kijiji cha Sukuro au kijiji cha Kitiangare. 

"Ni lazima sasa mgogoro huu wa muda mrefu ufikie tamati na wananchi na viongozi wa eneo hili wafanye shughuli za maendeleo na kuachana na suala hili linalorudisha nyuma maendeleo yenu," alisema Simbachawene. 

Awali, Waziri huyo aliagiza wananchi wa kitongoji cha Katikati, wapige kura ya kuchagua kuwa kwenye kijiji cha Sukuro au Kitiangare, jambo ambalo halikufanikiwa kwani baadhi ya watu walikuwa wananyoosha mikono mara mbili, wakiambiwa wachague kuwa Sukuro au Kitiangare. 

Mmoja kati ya wananchi wa eneo hilo, Rambo Sumuni alisema wanatarajia Waziri Simbachawene atatenda haki na kuidhinisha kitongoji hicho kuwa kwenye kijiji cha Sukuro kama ilivyopendekezwa mwanzo. 

Sumuni alisema hata gazeti la serikali (GN) inatambua kuwa kitongoji cha Katikati kipo kwenye kijiji mama cha Sukuro, ila ni baadhi ya wanasiasa wa wilaya hiyo kwa ajili ya maslahi yao walikwamisha utekelezaji wa suala hilo. 


Olendikoni Lembris alisema taratibu za kugawanya kilichokuwa kijiji cha Sukuro na kuwa vijiji viwili, zilifuatwa kwa kupitishwa kwa vikao kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, kata, wilaya hadi mkoa. 

Lembris alisema wananchi wa vitongoji walipitisha Katikati kuwa Sukuro na kikao cha maendeleo cha kata (WDC) kilipitisha, baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo walipitisha na kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) wakapitisha na kupelekwa Tamisemi walikopitisha kwenye gazeti la serikali. 

"Hata enzi ya Rais Jakaya Kikwete na DC wetu (aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo) Khalid Mandia, alikuja kwetu aliyekuwa Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika alishindwa kutatua hili suala na kuagiza kura zipigwe na wananchi waliogomea hilo ila nadhani Waziri Simbachawene ataliweza hili," alisema. 

Alisema ni jambo la kushangaza hatua zote zinazostahili zilipitisha suala hilo hadi kupata namba kupitia gazeti la serikali zilipitishwa, ila mwanasiasa mmoja kwa maslahi yake ya kuzusha mgogoro akaanzisha tatizo hilo lililokosa ufumbuzi. 

Mkazi wa eneo hilo, Lengai Ole Makoo alisema utaratibu wa kugawanywa kwa kijiji mama cha Sukuro, ulifuatwa kisheria na kitongoji cha Katikati kilipangiwa kujumuishwa katika kijiji cha Sukuro na siyo Kitiangare. 

Awali, miaka iliyopita vijiji vya Sukuro na Kitiangare vilikuwa ni kijiji kimoja kabla ya kugawanywa mwaka 2010 na kuwa vijiji viwili ambavyo hadi sasa vinagombea kitongoji hicho. 

Kijiji cha Sukuro kina vitongoji vinne vya Lenjani, Lembutwa, Lasepa na Mouwara na kijiji cha Kitiangare kina vitongoji vinne vya Lelero, Lodrepes, Laalarani na Langu. 

No comments:

Post a Comment