Wednesday, 23 August 2017

WACHIMBAJI MIRERANI WATAKIWA KUSALIMISHA MABOMU YA KUTENGENEZA KIENYEJI

 Wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanaojihusisha na mabomu ya kutengenezwa kienyeji, wameonywa vikali kwa kutakiwa wayasalimishe wenyewe kwenye kituo cha polisi Mirerani, kabla hawajachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa huo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Joshua Mwafulambo, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wamiliki na mameneja wa migodi ya madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani.

Mwafulambo alisema baadhi ya wachimbaji wanatengeneza mabomu ya kienyeji na kuyafanyia uhalifu kwenye migodi ya wenzao pindi wanapokuwa wametobozana na wenzao na kusababisha kuwe matatizo kwenye migodi hiyo.
Alisema matukio ya kurushiana mabomu ya kutengenezwa kienyeji kwenye migodi ya madini ya Tanzanite, yanapaswa kupingwa na kila mpenda amani hivyo mtu yeyote ambaye anafahamu analo bomu hilo alisalimishe mwenyewe polisi na hatachukuliwa hatua.

“Nimeagiza kwenye kituo cha polisi Mirerani kuwa yule ambaye atajitolea kurudisha mwenyewe mabomu ya kutengeneza asichukuliwe hatua yoyote, kwani ametekeleza kwa vitendo ile dhana ya utii wa sheria bila shuruti,” alisema Mwafulambo.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wa madini wa mkoa huo, (Marema) Sadiki Mneney alisikitishwa na baadhi ya wachimbaji kutoa maelezo kwa kamati ya Spika ya wabunge iliyofika hivi karibuni kwa kumtuhumu mkuu wa kituo cha polisi Mirerani Evarest Makala, kuwa aliingia mgodini na kusimamisha kazi.

Mneney alisema wao wana ushirikiano mkubwa na polisi, hivyo kitendo cha mkuu wa kituo cha polisi Mirerani kutuhumiwa jambo ambalo siyo la ukweli, linawavunja moyo askari hao ambao wamekuwa msaada mkubwa kwneye suala la ulinzi na usalama wa eneo hilo.

“Mtu anapozungumza mbele ya wabunge kuwa mkuu wa kituo cha polisi alizamia mgodini ili hali haikuwa hivyo, siyo vyema kwani inabidi mtu alaumiwe kwa kufanya makosa na siyo kusingiziwa jambo ambalo hajafanya,” alisema.

Katibu wa kamati ya ulinzi na usalama ya kitalu D, Salum Ngoya alisema suala la polisi kuingia mgodini siyo baya kwani polisi walishawahi kuingia mgodini na kuwakamata watu waliofanya uhalifu kwenye mikoa ya Mtwara na Mwanza waliokuwa wamejificha mgodini.

“Jamani tusilalamike pindi askari polisi watakapokuwa wanaingia migodini kwani mara nyingi inakuwa ni kwa faida yetu sisi wachimbaji kutokana na wakati mwingine tunakuwa tunafanya kazi na wahalifu bila kujua, lakini polisi wanakuja migodini na kuwakamata,” alisema Ngoya.

No comments:

Post a Comment