Wednesday, 23 August 2017

NILIJIITA MJOMBA HUSSEIN ILI NIZAME KWENYE MIGODI YA TANZANITE-PILI HUSSEIN

 Pili Hussein ni mmoja katiya wanawake wachache wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, waliobahatika kuwa na mgodi wa madini ya Tanzanite.
 
Akiwa mmiliki wa mgodi huo, Pili alibahatika kupata madini ya Tanzanite na kufanikiwa kuwekeza kwenye miradi mbalimbali na kujenga nyumba, kununua magari, mashamba, matrekta na pikipiki.

Kuchimba madini ni kazi ngumu ya shuruba yenye kuhitaji mitulinga, yeye ni mwanamke alifanikiwa kwa namna ipi kuzamia mgodini na kufanya kazi hiyo bila kugundulika kuwa ni mwanamke.

Pili Hussein ambaye anaelezea changamoto alizozipata mara baada ya kufika kwa mara ya kwanza miaka ya 80 kwenye machimbo hayo ya Tanzanite
 
Mwandishi:Ilikuaje ulipofika kwa mara ya kwanza kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite?

Pili: Wanawake walikuwa hawaruhusiwi kuzamia mgodini hivyo nikatamani kufanya shughuli hiyo ya kuchimba madini ili nipate fedha nyingi hivyo ilinibidi nibadili jina na kujiita mjomba Hussein kasha nikakata suruali zangu zikawa kaptula nikawa nazivaa na kuzamia mgodini.

Mwandishi: Baada ya hapo ikawaje?

Pili: Nilikuwa kama mwanaume kabisa kwani nilifunga panga kiunoni nikizamia mgodini umbali wa zaidi ya mita 100 chini ya ardhi kwenye vumbi, joto huku nikifanya kazi hiyo ngumu kama mwanaume halisi kumbe mimi ni mwanamke.

Mwandishi: Ulifanikiwa kupata madini ya Tanzanite ulipokuwa unachimba madini hayo?

Pili: Baada ya muda wa mwaka mmoja na miezi kadhaa nilipata utajiri wa madini hayo ya Tanzanite, kisha nikawajengea nyumba wazazi wangu mkoani Singida, ndugu zangu pia nikawajengea nyumba kisha nikaanzisha mgodi wangu binafsi ambao nao ulikuja kutoa madini nikanunua mashamba, magari, trekta, pikipiki na kujenga nyumba.
Mwandishi: Katika uchimbaji wako migodini, wachimbaji hawakuwahi kukuhisi kama wewe ni mwanamke?

Pili: Haikuwahi kutokea hivyo kwani hata sauti yangu ilikuwa ni kubwa ila siku moja ilitokea mwanamke alibakwa na watu kadhaa na polisi walipokuja kutukamata ndipo nikaeleza ukweli mtupu kwa kufika kituoni na kuwaomba askari wa kike wanikague kama nina uwezo wa kubaka na waliponiangalia ndipo wakabaini kuwa mimi ni mwanamke japo watu hawakuamini ila baadhi hawakuamini hadi nilipoolewa mwaka 1991 ndipo wakaamini.

Mwandishi:Kuna wanawake ambao wanazamia mgodini hadi hivi sasa?
Pili: Zaidi yangu mimi hakuna mwanamke ambaye anazamia mgodini kama mimi ila wapo wapishi migodini na ambao wanachekecha mchanga au udongo uliotoka mgodini ambao wanafanya shughuli hiyo juu mgodini ila hawaruhusiwi kuingia mgodini. 

Mwandishi: Unatoa wito gani kwa Serikali kuhusiana na kuwajengea uwezo wanawake wanaomiliki migodi, ambao wanachimba madini ya Tanzanite?

Pili: Serikali inapaswa kuwapa kipaumbele wanawake wanaomiliki migodi na kuchimba madini ya Tanzanite kwa kuwapatia mikopo kwani wengi wao wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa fedha za uendeshaji wa shughuli za migodini hasa sisi ambao migodi yetu haijatoa madini kwa muda mrefu.

WACHIMBAJI MIRERANI WATAKIWA KUSALIMISHA MABOMU YA KUTENGENEZA KIENYEJI

 Wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanaojihusisha na mabomu ya kutengenezwa kienyeji, wameonywa vikali kwa kutakiwa wayasalimishe wenyewe kwenye kituo cha polisi Mirerani, kabla hawajachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa huo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Joshua Mwafulambo, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wamiliki na mameneja wa migodi ya madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani.

Mwafulambo alisema baadhi ya wachimbaji wanatengeneza mabomu ya kienyeji na kuyafanyia uhalifu kwenye migodi ya wenzao pindi wanapokuwa wametobozana na wenzao na kusababisha kuwe matatizo kwenye migodi hiyo.
Alisema matukio ya kurushiana mabomu ya kutengenezwa kienyeji kwenye migodi ya madini ya Tanzanite, yanapaswa kupingwa na kila mpenda amani hivyo mtu yeyote ambaye anafahamu analo bomu hilo alisalimishe mwenyewe polisi na hatachukuliwa hatua.

“Nimeagiza kwenye kituo cha polisi Mirerani kuwa yule ambaye atajitolea kurudisha mwenyewe mabomu ya kutengeneza asichukuliwe hatua yoyote, kwani ametekeleza kwa vitendo ile dhana ya utii wa sheria bila shuruti,” alisema Mwafulambo.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wa madini wa mkoa huo, (Marema) Sadiki Mneney alisikitishwa na baadhi ya wachimbaji kutoa maelezo kwa kamati ya Spika ya wabunge iliyofika hivi karibuni kwa kumtuhumu mkuu wa kituo cha polisi Mirerani Evarest Makala, kuwa aliingia mgodini na kusimamisha kazi.

Mneney alisema wao wana ushirikiano mkubwa na polisi, hivyo kitendo cha mkuu wa kituo cha polisi Mirerani kutuhumiwa jambo ambalo siyo la ukweli, linawavunja moyo askari hao ambao wamekuwa msaada mkubwa kwneye suala la ulinzi na usalama wa eneo hilo.

“Mtu anapozungumza mbele ya wabunge kuwa mkuu wa kituo cha polisi alizamia mgodini ili hali haikuwa hivyo, siyo vyema kwani inabidi mtu alaumiwe kwa kufanya makosa na siyo kusingiziwa jambo ambalo hajafanya,” alisema.

Katibu wa kamati ya ulinzi na usalama ya kitalu D, Salum Ngoya alisema suala la polisi kuingia mgodini siyo baya kwani polisi walishawahi kuingia mgodini na kuwakamata watu waliofanya uhalifu kwenye mikoa ya Mtwara na Mwanza waliokuwa wamejificha mgodini.

“Jamani tusilalamike pindi askari polisi watakapokuwa wanaingia migodini kwani mara nyingi inakuwa ni kwa faida yetu sisi wachimbaji kutokana na wakati mwingine tunakuwa tunafanya kazi na wahalifu bila kujua, lakini polisi wanakuja migodini na kuwakamata,” alisema Ngoya.

SIMBACHAWENE AINGILIA KATI MGOGORO SIMANJIRO

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene ameingilia kati mgogoro wa muda mrefu wa kugombea kitongoji cha Katikati, baina ya vijiji viwili vya Sukuro na Kitiangare, vilivyopo kata ya Komolo, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Waziri Simbachawene amewapa ahadi ya muda wa wiki mbili, wananchi wa kata hiyo kuwa atamaliza mgogoro huo unasababisha migongano ya jamii ya eneo hilo, ambao kwa muda mrefu wengi wao wanaishi kwa kubaguana. 

Hadi hivi sasa kitongoji hicho hakina uongozi kutokana na mgogoro huo wa muda mrefu uliosababisha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Christopher Ole Sendeka (mkuu wa mkoa wa Njombe) na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Manyara, Henry Sheriff (Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga) kulumbana kwenye mkutano wa ndani. 

Waziri Simbachawene akizungumza kwenye mkutano wake na wananchi wa kata hiyo uliofanyika katika kijiji cha Sukuro, alisema baada ya muda huo mgogoro huo utamalizika ili ijulikane kitongoji hicho kitapelekwa kijiji cha Sukuro au kijiji cha Kitiangare. 

"Ni lazima sasa mgogoro huu wa muda mrefu ufikie tamati na wananchi na viongozi wa eneo hili wafanye shughuli za maendeleo na kuachana na suala hili linalorudisha nyuma maendeleo yenu," alisema Simbachawene. 

Awali, Waziri huyo aliagiza wananchi wa kitongoji cha Katikati, wapige kura ya kuchagua kuwa kwenye kijiji cha Sukuro au Kitiangare, jambo ambalo halikufanikiwa kwani baadhi ya watu walikuwa wananyoosha mikono mara mbili, wakiambiwa wachague kuwa Sukuro au Kitiangare. 

Mmoja kati ya wananchi wa eneo hilo, Rambo Sumuni alisema wanatarajia Waziri Simbachawene atatenda haki na kuidhinisha kitongoji hicho kuwa kwenye kijiji cha Sukuro kama ilivyopendekezwa mwanzo. 

Sumuni alisema hata gazeti la serikali (GN) inatambua kuwa kitongoji cha Katikati kipo kwenye kijiji mama cha Sukuro, ila ni baadhi ya wanasiasa wa wilaya hiyo kwa ajili ya maslahi yao walikwamisha utekelezaji wa suala hilo. 


Olendikoni Lembris alisema taratibu za kugawanya kilichokuwa kijiji cha Sukuro na kuwa vijiji viwili, zilifuatwa kwa kupitishwa kwa vikao kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, kata, wilaya hadi mkoa. 

Lembris alisema wananchi wa vitongoji walipitisha Katikati kuwa Sukuro na kikao cha maendeleo cha kata (WDC) kilipitisha, baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo walipitisha na kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) wakapitisha na kupelekwa Tamisemi walikopitisha kwenye gazeti la serikali. 

"Hata enzi ya Rais Jakaya Kikwete na DC wetu (aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo) Khalid Mandia, alikuja kwetu aliyekuwa Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika alishindwa kutatua hili suala na kuagiza kura zipigwe na wananchi waliogomea hilo ila nadhani Waziri Simbachawene ataliweza hili," alisema. 

Alisema ni jambo la kushangaza hatua zote zinazostahili zilipitisha suala hilo hadi kupata namba kupitia gazeti la serikali zilipitishwa, ila mwanasiasa mmoja kwa maslahi yake ya kuzusha mgogoro akaanzisha tatizo hilo lililokosa ufumbuzi. 

Mkazi wa eneo hilo, Lengai Ole Makoo alisema utaratibu wa kugawanywa kwa kijiji mama cha Sukuro, ulifuatwa kisheria na kitongoji cha Katikati kilipangiwa kujumuishwa katika kijiji cha Sukuro na siyo Kitiangare. 

Awali, miaka iliyopita vijiji vya Sukuro na Kitiangare vilikuwa ni kijiji kimoja kabla ya kugawanywa mwaka 2010 na kuwa vijiji viwili ambavyo hadi sasa vinagombea kitongoji hicho. 

Kijiji cha Sukuro kina vitongoji vinne vya Lenjani, Lembutwa, Lasepa na Mouwara na kijiji cha Kitiangare kina vitongoji vinne vya Lelero, Lodrepes, Laalarani na Langu. 

SIMBACHAWENE AIMWAGIA SIFA SIMANJIRO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene amezitaka wilaya nyingine kuiga wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara kwa namna ilivyojenga majengo ya madarasa, maabara na nyumba za walimu kwa ubora na thamani ya fedha zilizotengwa. 

Waziri Mkuchika akizungumza kwenye ziara yake ya siku moja Wilayani Simanjiro alipitia katika shule ya sekondari Loiborsiret Wilayani Simanjiro alisema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwani majengo yamesimamiwa vizuri na kujengwa kwa ubora unaotakiwa. 

Alisema viongozi wa wilaya nyingine nchini wanapaswa kupata somo kupitia ujenzi huo ambao thamani ya fedha inaendana na thamani ya ujenzi wa miundombinu iliyofanyika kwenye shule hiyo ya sekondari. 

Alisema baadhi ya maeneo unakuta viongozi wanashindwa kusimamia vyema na kujenga majengo ya shule yenye ubora, ambayo baada ya muda mfupi yanaweka nyufa na yanabomoka. 

"Pamoja na hayo nawapongeza pia wanafunzi wa shule hii ambao wengi wao ni jamii ya kifugaji wa kimasai ambao baadhi yao nimekagua madaftari yao na kubaini kuwa kiwango cha taaluma ni kizuri tofauti na matarajio yangu, hongereni sana walimu wa shule hii," alisema Simbachawene. 

Alisema walimu wa shule hiyo wanastahili pongezi nyingi kwa kufanya kazi yao kwa uadilifu na pia wanafunzi nao kwa upande wao wanafunzi wanatimiza wajibu wao kwa kusoma ipasavyo. 

Mhandisi wa ujenzi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Martin Mwashambwa alisema ujenzi huo umegharimu kiasi cha sh219.9 milioni, pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT). 

Mhandisi Mwashambwa alisema ujenzi huo umehusisha nyumba kubwa yenye uwezo wa kuishi familia sita iliyogharimu sh149.9 milioni na vyumba viwili vya madarasa vya thamani ya sh49.6 milioni. 

Mhandisi huyo alitaja ujenzi mwingine ni vyoo vya wanafunzi wa shule hiyo uliohusisha matundu nane yenye thamani ya sh20. 3 milioni. 

Mkuu wa wilaya hiyo, mhandisi Zephania Chaula alimshukuru Waziri Simbachawene kwa pongezi hizo alizozitoa kwao kutokana na ubora wa ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo ya sekondari Loiborsiret. 

"Mheshimiwa Waziri, ukiwa na mkuu wetu wa mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera, nakuhakikishia kuwa hatutalala usingizi na kubweteka kwa sifa hizo ila tutaongeza juhudi zaidi juu ya ujenzi bora wa majengo ya serikali," alisema mhandisi Chaula. 

UTUNZAJI MAZINGIRA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Hamis Malinga (wapili kulia) akikagua vitalu vya miche ya utunzaji mazingira kwenye kijiji cha Sarame.

Sunday, 20 August 2017

MAGAZETI YA JUMAPILI LEO AGOSTI 20, 2017

MABASI MAWILI YAGONGANA MBULU

 Mkuu wa Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga akikagua ajali ya mabasi ya kampuni ya Manday Trans na Neema ya Mungu, iliyotokea kwenye daraja la Kijiji cha Masqaroda na kusababisha watu 20 kujeruhiwa ila hakukuwa na vifo, majeruhi hao wamelazwa kwenye hospitali ya wilaya ya Mbulu na wengine watatu wamelazwa hospitali ya rufaa ya Haydom inayomilikiwa na KKKT
Basi la kampuni ya Manday Trans baada ya ajali hiyo
 Basi la Neema ya Mungu baada ya ajali hiyo
 Mkuu wa Wilaya ya Mbulu na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Paul Bura wakiwa wamewatembelea majeruhi wa ajali hiyo kwenye hospitali ya Mbulu
Mmoja kati ya majeruhi wa ajali hiyo.