Sunday, 8 June 2014

WACHIMBAJI WA TANZANITE KUTOFUTIWA LESENI ZAO WALIOPAKANA NA TANZANITEONE

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana amesema Serikali imesitisha uamuzi wa kufuta leseni ya migodi 18 ya madini ya Tanzanite ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro inayopakana na kampuni ya TanzaniteOne.
 
Akizungumza na wananchi wa Mirerani wakati akihitimisha ziara yake, Kinana alisema ameshawasiliana na Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo na amemdhibitishia kuwa zoezi hilo lililotakakufanya na Kamishna wa madini Kanda ya kaskazini Alex Magayane limesitishwa.
 
Kinana alisema Kamishna wa madini nchini Paul Masanja atatembelea machimbo hayo na kuzungumza na wachimbaji wadogo na pia Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini itakutanana wachimbaji hao.
 
Aliwataka wachimbaji hao kujipanga kwa hoja ili kufikisha kilio chao cha muda mrefu kuwa wananyanyaswa, kwani machimbo hayo yaliyoanzishwa mwaka 1967 yanawanufaisha wachimbaji wadogo hivyo ni tegemeo lao kiuchumi.
 
“Jipangeni vizuri, andaeni mambo yenu yote na siyo watu hao wanakuja hapa kisha mnaanza kulalamika ohoo tulishawahi kupigwa risasa mara tunamwagiwa maji, ohoo tunang’atishwa mbwa, jengeni hoja ndugu zangu,” alisema Kinana.
 
Hata hivyo, Katibu mkuu huyo alishangazwa na kitendo cha kupitishwa sheria ya madini ya mwaka 2010 inayowataka wachimbaji wa madini ya Tanzanite kuchimba wima (Vetical) badala ya mshazari (Horizontal).
 
“Kwa jiolojia ya madini ya Tanzanite, huwezi kuyachimba kama unavyotaka kuchimba choo, ni lazima uende kulia, kushoto, chini, juu na ndiyo sababu ya jina nyoka kupatikana, yaani kona kona, sheria hiyo inaumiza,” alisema Kinana.
 
Naye, mbunge wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka alisema yeye siyo mchochezi na ataendelea kutetea maslahi ya wachimbaji wa madini kwani ndiyo walimchagua ili awawakilishe Bungeni na siyo vinginevyo.
 
“Ndugu Katibu Mkuu nitaendelea kutetea maslahi ya wachimbaji wadogo hadi mwisho wa ubunge wangu na mwisho wa uhai wangu, kwani natetea maslahi yao kwa vile hawana sauti ya kuwasemea,” alisema Ole Sendeka.
 
Alisema Rais Jakay Kikwete alitoa ahadi ya kuwapatia eneo la machimbo ya Tanzanite kitalu B, iliyo kampuni ya TanzaniteOne pindi leseni yao itakapomalizika ila ameshangazwa na kampuni hiyo kupewa kipindi kingine.  
 

No comments:

Post a Comment