Mtoto wa jamii ya kifugaji wa Kijiji cha
Ndaleta, Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, amepatwa na ugonjwa wa kichaa cha
mbwa, baada ya kung’atwa na mbwa na daktari aliyemtibu kudaiwa kumpiga sindano
ya kuzuia pepo punda badala ya kumpa tiba ya kung’atwa na mbwa.
Baba wa mtoto huyo, Loshiye Koronya, akizungumza kwenye hospitali ya wilaya ya Kiteto, baada ya madaktari kumuhakikishia
kuwa mtoto wake Mgeno Koronya (3) hatapona, alielekeza malalamiko yake kwa
daktari aliyempa dawa.
Koronya alisema daktari wa zahanati ya Njoro
wilayani humo (jina tunalo) alimdai sh90,000 ambazo alimpatia ili amtibu mtoto
wake, lakini badala ya kumpa tiba sahihi yeye akamchoma sindano ya kuzuia pepo
punda.
Alisema mtoto wake aling’atwa na mbwa mwanzo mwa
mwezi Mei mwaka huu, kisha akampeleka mtoto huyo kwenye zahanati hiyo ili
apatiwe matibabu lakini Mei 15 Mgeno akazidiwa na kupata ugonjwa wa kichaa cha
mbwa.
“Madaktari wamenihakikishia kuwa mwanangu
hatapona na akiishi zaidi ya siku tatu nimshukuru Mungu, ila huu ni uzembe wa
dokta Steve ambaye alichukua fedha zangu lakini hakumtibu ipasavyo mtoto
wangu,” alisema Koronya.
Alisema baada ya Mgeno kupata ugonjwa wa kichaa
cha mbwa, daktari huyo alidai kuwa huenda mbwa aliyemng’ata, naye aling’atwa na
fisi kwani dawa alizompatia zingemaliza tatizo hilo lakini haikuwa hivyo.
Hata hivyo, Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya
Kiteto, Dk Leadry Malisa alithibitisha Mgeno kupata kichaa cha mbwa, kwani
dalili zote za kuogopa maji na kuwa na mate mengi mdomoni anazo, hivyo kupona
kwake ni bahati.
“Inaonyesha virusi vimeshafika kichwani na
kupona kwake ni kazi sana, huenda tatizo hili limesababishwa na kutohifadhiwa
vizuri kwa sindano iliyotumika au dawa iliyotumika kumtibu siyo yenyewe,”
alisema Dk Malisa.
Alisema atafuatilia suala hilo kwenye zahanati
hiyo ya Njoro kwa kupata maelezo ya daktari huyo aliyempa huduma mtoto huyo,
baada ya kung’atwa na mbwa, ili kubaini sababu iliyofanya hali hiyo imtokee
Mgeno.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Kibaya
waliomuona mtoto huyo akiwa hospitalini hapo walisikitishwa na kitendo hicho
kwani kila wakati mtoto huyo alikuwa anapiga kelele na wakaiomba Serikali
imchukulie hatua mganga huyo.
No comments:
Post a Comment