Utumikishwaji wa watoto wenye umri chini ya miaka 18
(nyoka) kwenye migodi ya madini ya Tanzanite, Mji mdogo wa Mirerani Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara, hivi sasa haupo katika migodini hiyo, imeelezwa.
Hayo yalielezwa na Ofisa maendeleo ya jamii wa mji
mdogo wa Mirerani, Isack Mgaya ambaye alidai kuwa alitembelea migodi 49 ya
madini ya Tanzanite na kuzungumza na viongozi wa migodi hiyo juu ya kupiga vita
ajira za watoto.
“Tulichunguza na kutembelea ili kuikagua migodi tofauti,
ambapo tulikutana na mameneja na wamiliki wa migodi, ambao kwa kiasi kikubwa
walituelewa na tuliwaeleza kuwa ni kinyume cha sheria kutumikisha watoto,”
alisema Mgaya.
Alisema kuwa baada ya kuchunguza na kujiridhisha kuwa
hakuna ajira ya watoto kwenye migodi hiyo ya Tanzanite, walitoa elimu kwa
mameneja 19 juu ya utumikishwaji watoto na wakaunga mkono jitihada hizo kwa
kutowaajiri.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo wa
madini mkoani Manyara, (Marema) Tawi la Mirerani, Japhary Matambi alikanusha
vikali kutumika kwa watoto (nyoka) kwenye migodi ya madini ya Tanzanite.
“Hili jambo tumeshalipiga marufuku na tulishawaeleza
wachimbaji wa madini ya Tanzanite kuwa mtu akikutwa anamtumikisha mtoto kwenye
mgodi wake, atapigwa faini ya sh500,000 hivyo hilo jambo halipo huku,” alisema
Matambi.
Miaka ya mwanzoni mwa mwaka 2000 kulikuwa na zaidi ya
watoto 100 waliokuwa wanafanya kazi kwenye migodi hiyo, ila kutokana na
jitihada za asasi ya Good hope chini ya mkurugenzi wake Dorah Mushi, ajira hizo
zilisitishwa.
Kupitia Good hope watoto hao walikusanywa na wengine
kurudishwa shule za msingi kusoma huku baadhi yao wakipelekwa kufundishwa
ufundi mbalimbali ikiwemo wa useremala, magari, pikipiki na hadi sasa
wanaendelea na kazi hizo.
No comments:
Post a Comment