Sakata la Mbunge wa Viti maalumu wa
Mkoa wa Manyara, (Chadema) Pauline Gekul kudai kufanyiwa vurugu na Mkurugenzi
wa Mji wa Babati, Omary Mkombole na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mohamed
Farah limechukua sura mpya baada ya mbunge huyo kufungua kesi polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Gekul alisema amefungua kesi namba 606/2014 polisi Babati ya shambulio,
kudhalilishwa, kuporwa fedha sh5 milioni na kufanyiwa fujo na viongozi hao
wawili wa mji huo.
Alidai kuwa viongozi hao walimfanyia
vitendo hivyo ikiwemo kumchania blauzi wakati wakimpokonya nyaraka
zilizoonyesha uchakachuaji wa majina ya watu wanaodai fidia kwenye shamba la
katani la Siratu kwenye kikao cha kamati ya Mipango na Mazingira.
“Nimefungua kesi na tutakutana
Mahakamani kwani huo ni udhalilishaji wao ni wanaume na mimi mwanamke isitoshe
mimi nina hadhi ya kidiplomasia sipekuliwi hovyo hovyo,” alisema Gekul.
Hata hivyo, Kamanda wa polisi wa mkoa
wa Manyara alithibitisha jana kuwa mbunge huyo kufungua malalamiko yake kwenye
kituo cha polisi Babati na wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Kwa upande wao, Farah na Mkombole kwa
mujibu wa taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana wamekanusha vikali
kumfanyia fujo, kumdhalilisha na kumpora fedha mbunge huyo.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkombole
imedai kuwa chanzo cha kumnyanganya Gekuli nyaraka hizo ni tabia yake ya
kuondoka nazo na kuzitumia kwenye vyombo vya habari na kwenye mikutano ya
wananchi.
“Amefanya kosa kuondoka na nyaraka
kwani ni kinyume na kanuni ya 51 ya vikao vya ndani vya kamati mbalimbali
isipokuwa vikao vya Baraza tu na wananchi na vyombo vya habari wanaruhusiwa
kuingia” alisema Mkombole.
Alisema awali, wajumbe wote wa kamati
ya Mipango miji na mazingira ambapo Gekul ni mjumbe walitii agizo la kurudisha
nyaraka kasoro mbunge huyo peke yake alitaka kuondoka nazo.
“Juhudi za kumshawishi arudishe
nyaraka hizo zilishindikana kwani aligoma ndipo Mwenyekiti wa halmashauri
akamnyanganya nyaraka hizo kumkabidhi Mkurugenzi na hapakuwa na purukushani
wala hakupigwa wala kuchukuliwa chochote,” alisema Mkombole.
Alisema kuwa Gekul ni mjumbe halali
wa vikao vya halmashauri ya mji huo na anataarifiwa na kuhudhuria mchango wake
mjini Babati ila anawajibika kama kiongozi kutii na kulinda heshima kwa
viongozi na wananachi anaowawakilisha.
Tukio hilo la kushambuliwa kwa mbunge huyo lilitokea juzi saa 12 jioni katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Babati, mara baada ya kikao kilichokuwa kikifanyika chini ya mkurungenzi huyo kumalizika.
Akizungumza mara baada ya kutoka polisi jana kutoa maelezo juu ya vurugu hizo, Gekul alisema kikao hicho kilichosababisha vurugu hizo, kilikuwa kinajadili mustakabali wa ugawaji wa shamba la Sisal Plantation lenye ekari 4200.
Alisema shamba hilo wakulima walilipia mwaka 2000 na Baraza la Madiwani lilikwishatoa uamuzi wa kugawanywa, lakini juzi katika orodha iliyotolewa, alibaini majina mengi yameghushiwa na walengwa wengi hawapo na baada ya viongozi wa halmashauri kubaini amegundua njama hizo, ndipo waliagiza kurejeshwa makabrasha yote.
“Mimi nilikataa kwa sababu orodha hii ina makosa na mimi nawafahamu baadhi ya wakulima wanaopaswa kupewa eneo hili “alisema Gekul.
Alisema Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mohammedi Fara
baada ya yeye kukataa kurejesha, aliahirisha kikao na walipotaka kutoka nje ghafla alitokea Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Omari Mkombole ambaye alidai alikwenda Polisi kufuatilia suala la wakulima hao na tayari wanataka kuendesha msako wa waliovamia eneo hilo bila idhini ya halmashauri.
“Lakini cha ajabu baada ya kusema hivyo, mkurugenzi huyu akanifuata na kunikaba kwa nguvu, kisha kunichania nguo zangu na kunipokonya karatasi akidhani zina majina ya wakulima hao,
Alisema baada ya mlango kufungwa alianza kupokonywa kwa nguvu pochi yake na wakachambua ndani na kuondoka na nyaraka zote, huku ufunguo wa gari ukitupwa.
No comments:
Post a Comment