Wazee wa jamii ya kifugaji wa kimasai (Malaigwanan) wa Kata
ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameunga mkono kitendo cha
wananchi wa Kijiji cha Kambi ya Chokaa kumsimika Joshua Kuney kuwa Mwenyekiti
wa Kijiji hicho.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wazee hao walisema
wananchi hao walichukua uamuzi sahihi wa kumsimika Kuney kwani alishinda kura ya
maoni ya CCM kwa kupata kura 335 dhidi ya Mbuki Mollel aliyepata kura 215.
Desemba 14 mwaka huu, wananchi wa kijiji hicho walimsimika
Kuney kuwa Mwenyekiti wa kijiji hicho baada ya uongozi wa CCM wilaya hiyo
kukata jina lake na kumpitisha Mollel ambaye alishika nafasi ya pili.
Mmoja kati ya wazee hao Kisota Lengitambi (74) alisema
malaigwanan wanaunga mkono uamuzi wa wananchi hao kwani wamemsimika mtu
waliyemchagua wao na siyo chaguo la viongozi wa CCM wilaya hiyo.
“Nawapongeza wananchi kwani hawa viongozi walitaka kuleta
vurugu na kuhatarisha amani kwenye kijiji cha Kambi ya Chokaa, kwani wananchi
walimchagua mtu wanayempenda wao na siyo huyo Mollel chaguo la wilaya,” alisema
Lengitambi.
Naye, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Naisinyai Mosses Makeseni
alisema kitendo cha wilaya kukata jina la mshindi na kumpitisha aliyeshindwa ni
kudharau uamuzi wa wananchi wenye maamuzi sahihi na yenye busara.
“Walitaka kuhatarisha hali ya amani kwenye eneo hili ila wananchi
walikuwa wavumilivu na kuchukua uamuzi wa busara, hivyo viongozi waliosababisha
hali hiyo inatakiwa wachukuliwe hatua,” alisema Makeseni.
Alisema hawatambui huyo Mollel chaguo la wilaya anawaza
kufanya jambo gani kwani yupo mafichoni na hajawahi kufika kwenye kijiji hicho
tangu tukio hilo lifanyike na kuwapa wananchi wasiwasi wa kutotambua mustakabali
huo.
Hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndengaso
Ndekubali ambaye aliwaagiza viongozi wa CCM wilaya ya Simanjiro kumpitisha
Kuney ambaye ni chaguo la wananchi na agizo hilo kutotekelezwa alisema atatoa
uamuzi kuhusu hilo
hivi karibuni.
“Kama wananchi wameamua kufanya jambo hilo kwa kumsimika
yeye kuwa kiongozi wao baada ya kumchagua nitatoa tamko la CCM mkoa hivi
karibuni ili kuhakikisha suala hilo linakuwa katika hali nzuri zaidi,” alisema
Ndekubali.
No comments:
Post a Comment