Friday 26 December 2014

MAREMA WAOMBA HISA



Mussa Juma Mwananchi

Arusha. Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini cha Manyara (Marema) kimeitaka Serikali kukipa asilimia 50 ya hisa zake katika migodi ya TanzaniteOne iliyopo Mirerani na kuipongeza kampuni ya wazawa ya Sky Associates Group (LTD) kwa kununua asilimia nyingine 50 ya hisa.

Mwenyekiti wa Marema, Sadiki Mnenei alisema ofisini kwake juzi kuwa kampuni hiyo ya wazawa ambayo imenunua hisa kwa Sh32 bilioni, imeonyesha jinsi wazawa walivyo na uwezo wa kuwekeza wakipewa nafasi na kuondoa dhana kuwa hawana uwezo.

“Sisi tunawapongeza wenzetu kwa kununua asilimia 50 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na kampuni ya Richland Resources ya England ndani ya TanzaniteOne katika migodi ya kitalu C ya machimbo ya Tanzanite na tunataka tupewe hisa zilizobaki,” alisema.

Alisema sheria ya madini ya vito, inaeleza wazi madini hayo yatachimbwa na wazawa, umefika wakati kwa Serikali kuachia asilimia 50 ya hisa hizo kwa wazawa badala ya kuzipeleka kwa shirika la Stamico ambalo alidai kuwa lina majukumu mengi. 

“Wanachama wetu wana uwezo, tupewe asilimia 50 na tupo tayari kuzinunua ili kilio cha miaka mingi cha wachimbaji wadogo kiwe kimepatiwa ufumbuzi,” alisema.

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Sky associated Group Ltd, Faisal Shahbhai alisema wako tayari kufanya kazi na wadau wote wa madini ya tanzanite katika kuhakikisha Watanzania wananufaika na madini hayo.

“Sisi tunaomba ushirikiano na wadau wote wa madini ili tuweze kuongeza uzalishaji wa madini haya pia kuibua masoko mapya ya uhakika ndani na nje ya nchi,” alisema.

Kampuni ya TanzaniteOne ilikuwa inamiliki leseni ya uchimbaji madini (SML 8/92) kwa asilimia 100 kabla ya Serikali kuingia ubia kupitia Stamico ambayo bado inamiliki asilimia 50 ya hisa kutokana na kutekeleza matakwa ya kisheria ya uchimbwaji wa madini ya vito.

No comments:

Post a Comment