Friday 10 November 2017

WACHIMBAJI WAKUTANA GEITA KUMNYANYUA ZAIDI MCHIMBAJI MDOGO

 Mkuu wa Mkoa wa Geita Robert Luhumbi amewataka wadau wa madini kuhakikisha sekta hiyo inaakisi maendeleo ya jamii inayozunguka eneo hilo ili waone faida ya kuwepo kwa rasilimali hiyo muhimu. 

Luhumbi aliyasema hayo mjini Geita kwenye ufunguzi wa majadiliano ya wachimbaji wadogo Tanzania yaliyowashirikisha wadau wa madini wa nchi mbalimbali duniani. 

Akizungumza kabla ya washiriki hao hawajaanza safari ya kutembelea migodi ya madini ya dhahabu, Luhumbi alisema faida ya uwepo. 
 Alisema uwepo wa rasilimali ya madini ya dhahabu mkoani Geita bado haujaonekana ipasavyo kwa jamii ya eneo hilo kwani zinapaswa kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, maji, elimu, afya na mengineyo. 

"Hatutaki kuona rasilimali ya madini inaoneka kuwa ni laana kwa jamii badala ya baraka, kwani kupitia tunu hiyo wananchi wanapaswa kunufaika kwa kuona maendeleo yanafanywa kwenye maeneo hayo," alisema Luhumbi. 

Alisema sekta ya wachimbaji wadogo wa madini inafanywa na idadi ya watu milioni moja hadi milioni moja na nusu nchini hivyo wanapaswa kuwekewa mazingira rafiki yatakayoboeesha maisha yao. 

 Mkurugenzi wa asasi ya Haki Madini, Amani Mhinda alisema wameandaa mdahalo huo kwa uwezeshwaji wa taasisi ya kimataifa ya mazingira (IIED) kituo cha kimataifa cha utafiti wa misitu (CIFOR) na kampuni ya ushauri ya MTL. 

Mhinda alisema lengo ni kutoa suluhu juu ya changamoto zinazomkumba mchimbaji mdogo nchini na kupendekeza majawabu. 

Alisema sekta ya uchimbaji madini nchini ni kati ya sekta zinazokua kwa kasi kubwa na yenye mchango mkubwa wa uchumi wa Taifa. 

Alisema ingawa mipango mahususi ya kisera juu ya uchimbaji mdogo imeanzishwa, bado kuna changamoto nyingi hasa katika uelewa, ujasiri, mipango, fedha na taratibu zinazokwamisha utekelezaji wa sera na maboresho. 

 Mchimbaji wa madini wa kampuni ya Nsangano Gold mine, Renatus Nsangano alisema bado wachimbaji wadogo wana changamoto ya kufanya kazi bila kufanya utafiti. 

Nsangano alisema endapo wangekuwa wanafanya utafiti na kubaini madini yalipo ingekuwa na tija kubwa kwa wachimbaji wengi. 


Hata hivyo, alisema wamesaidia jamii zinazowazunguka kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya elimu, afya na maji. 


No comments:

Post a Comment