Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa Baraza Kuu la
Chadema, Edward Lowassa, amemshukia Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo kuwa
asitafute umaarufu wa kisiasa kwa kutumia jina lake.
Akizungumza jana kwenye mkutano wa kampeni ya
kumnadi Joyce Rutha (Chadema) mgombea udiwani wa kata ya Makiba Wilayani
Arumeru Mkoani Arusha, Lowassa alisema hujatuma watu kwa Gambo ili arudi
CCM.
Alisema kuendelea kumzungumzia Gambo kwenye majukwa ya kisiasa ni kumpa umaarufu wa bure kwani yeye hujamtuma mtu au watu kutoka Monduli ili aende kwa mkuu huyo wa mkoa kwa lengo la kuomba arudi CCM.
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo jana
kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na tweeter,
aliandika kuwa amepokea ujumbe kutoka Monduli.
Gambo aliandika kuwa ujumbe huo ulikuwa na
ombi moja kubwa amuombee mzee wa Monduli kwa Rais Magufuli ili akubali kumuona
na yeye yupo tayari kurudi nyumbani kama Rais atakubali kumuona.
Alisema ujumbe huo unasema ombi hilo katuma
muda mrefu bila majibu.
"Mnao mfahamu mzee huyu mfikishieni
ujumbe kuwa salamu nitaifikisha, mjumbe hauwawi," aliandika Gambo.
Lowassa alisema jana mchana alisoma kwenye
mitandao ya kijamii kuwa ametuma watu wamuombee ili arudi CCM jambo ambalo siyo
kweli.
"Siwezi kumjibu huyu kijana kwani
kuendelea kumjadili ni kumpa umaarufu hivyo simjibu chochote kwenye hilo,"
alisema Lowassa.
Akizungumza wakati wa kumnadi mgombea udiwani
huyo, Lowassa aliwataka wananchi wa kata ya Makiba kumpa kura nyingi za ndiyo
Rutha ili awe diwani wao.
"Mwaka 2015 nilikuja kuwaomba kura na
mkanipa kwa wingi sasa endeleeni kuikataa CCM kwa kumpa kura mgombea wetu wa
Chadema Rutho," alisema Lowassa.
Pia, alisema wananchi zaidi ya milioni sita
waliompigia kura nao wanapaswa kusemewa na wao kwa kuwepo kwa serikali ya
mseto.
Alisema katiba mpya ni jibu kwa kuweka
kipengele cha serikali ya mseto kwa mlengo wa kushoto na kulia ili mtu mmoja
asipate nafasi ya kuharibu vitu vingi.
Alisema hata Marekani na Ufaransa
wanashirikiana kwenye nafasi hizo pindi uchaguzi ukifanyika bila kujali chama
ni cha kijamaa au kibepari.
"Japo kuna wabunge lakini wale watu
milioni sita walionipigia kura nao wanapaswa kuwakilishwa serikali kama wale
milioni nane wengine ambao wana mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya,
wakurugenzi na viongozi wengine," alisema Lowassa.
Nassari alisema wananchi wanapaswa kumchagua
Rutha bila kujali kabila lake kwani jambo la muhimu ni kusimamia
maendeleo.
Alisema Rutha ni mgombea mwadilifu kwani
wapinzani wao waliweza kumrubuni kwa sh5 milioni na kumwekea pingamizi lakini
tume ikamrudisha.
Ole Millya alisema anashangazwa na watu
waliokuwa Chadema kisha wanarudi CCM ili hali hakuna jambo kubwa walilofanyiwa
hadi kusababisha kuachana na chama hicho zaidi ya tamaa.
"Ni kwa furaha gani wewe Mollel unarudi
CCM, ili hali wafugaji wanaendelea kuteseka kote Tanzania, jibu la yote hayo ni
kuendelea kuwa Chadema na siyo kukimbia," alisema Ole Millya.
Mgombea udiwani wa kata hiyo Joyce Rutha
alisema endapo atachaguliwa kuwa diwani, atahakikisha anakuwa mwakilishi mwema
wa wananchi wa eneo hilo kwenye halmashauri ya wilaya hiyo.
Rutha alisema ataendelea kufanya kampeni ya
nyumba kwa nyumba ili ahakikishe Chadema inashinda kwenye nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment