Friday 10 November 2017

RC MNYETI ATEMBELEA UKUTA MIRERANI

  Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, ameanza rasmi kazi Mkoani humo kwa kukagua ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli. 

Mnyeti alitembelea eneo hilo na mwenyeji wake mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo. 

Alipongeza kasi ya maandalizi ya ujenzi huo kwani kila sehemu aliyokagua ambapo ukuta utapita aliwakuta vijana hao wa JKT wana ari na hamasa ya utendaji kazi. 

"Kwa namna vijana wetu wanajeshi wanavyoonekana kwenye maeneo yote niliyopitia wanaonyesha wataimaliza kazi hii ndani ya muda mfupi tofauti na agizo la miezi sita lililotolewa na Rais Magufuli," alisema Mnyeti.

Aliwaahidi kutoa ushirikiano kwa jambo lolote lile watakalokuwa wanalitaka kwenye serikali ili kuhakikisha agizo hilo la Rais Magufuli linatekelezeka kwa wakati husika. 
 Kamanda wa operesheni ukuta Mirerani, Kanali Festus Mang'wela alimhakikishia mkuu huyo wa mkoa kuwa vijana wote wanaojenga ukuta huo watafikishiwa ujumbe wa kujikinga na maambukizi ya VVU kwa lengo la manufaa ya kulinda afya zao. 

Kanali Mang'wela alisema ukuta huo  wenye kilometa 24.5 na urefu wa mita tatu kwenda juu umeanza kujengwa rasmi Novemba 6 mwaka huu. 

Alisema mkuu wa JKT Meja jenerali Michael Isamuhyo ndiye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo wa ukuta wanaotarajia kuujenga kwa muda usiopungua miezi sita. 

Alitoa shukrani kwa serikali ya wilaya ya Simanjiro kwa ushirikiano mkubwa wanaowapa askari hao wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa ukuta huo.
Katibu Tawala wa wilaya ya Simanjiro, Zuwena Omary akisoma taarifa ya Wilaya hiyo kwa mkuu wa mkoa huo alisema wanashirikiana ipasavyo katika maandalizi ya ujenzi wa ukuta huo. 

Alisema serikali ya wilaya ya Simanjiro na uongozi wa JWTZ wamekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika ipasavyo na kwa wakati muafaka. 

Alisema ukuta huo utachangia kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo ambayo huuzwa yakiwa ghafi au kusanifiwa na kuuzwa na madalali na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi. 

Alisema katika utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli, wamefanikisha uanzishwaji wa ujenzi wa ukuta na kupatikana eneo la mnada wa madini ya Tanzanite Mirerani. 

"Hadi hivi sasa imeshafanyika minada minne ya madini ya Tanzanite jijini Arusha na serikali kuu na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro zikapata kodi ya mapato na kodi ya huduma ila minada ijayo itafanyika Mirerani," alisema Omary. 


No comments:

Post a Comment