Sunday, 25 November 2012

MAJI GALAPO KASHESHE

TATIZO la muda mrefu la uhaba wa maji kwa wakazi wa kijiji cha Galapo Wilayani Babati Mkoani Manyara limesababisha kuvunjika kwa mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe baada ya waziri huyo kuwakejeli wapinzani kuwa hawawezi kuwapa maji wananchi hao.

Hali hiyo ilijitokeza juzi kijijini hapo ambapo Prof Magembe alifika eneo hilo na kutegemewa na wananchi kuwa atavunja Mamlaka ya maji safi na maji taka Galapo (Gawasa) wanaodaiwa kuchukua fedha lakini hawatoi huduma ya maji.

Awali,waziri huyo alizungumza na wakazi hao na kudai kuwa ni lazima wananchi wachangie huduma ya maji ili mamlaka ziweze kununua vifaa vinavyohitajika katika kuendesha miradi husika,kwani hiyo ndiyo sera ya Serikali ya CCM.

“Naagiza kuwa maji yatalipiwa ili huduma iwe endelevu na agizo hili pia nalielekeza kwa mamlaka za maji za miji midogo yote nchini iwe Galapo,Dareda,Magugu na Bashnet,” alisema Prof Maghembe.

Hali ya mkutano huo,ilibadilika baada ya waziri huyo kudai kuwa wapinzani wanakuwa na maneno mengi lakini ukiwaambia watekeleze jambo lolote wana shindwa na kubaki kuilaumu CCM.

“Hawa wapinzani kama ni matusi wacha wanitukane tu lakini suala la kuwapa maji eneo hili hawawezi ni kelele tu za bure nyie endeleeni kuchangia maji mnayotumia kwani ndiyo sera yetu,” alisema Prof Maghembe. 

Kauli hiyo iliamsha nyongo za wakazi hao zilizolala,kwani baadhi yao walianza kuonyesha vidole viwili hewani na kudai kuwa wapinzani wataweza  kuleta maji kwani kuna baadhi ya maeneo wameweza.

Baadhi yao walipasa sauti na kudai kuwa Chadema ina uwezo wa kuleta maji kwani mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki,Joshua Nassari aliweza kuwachimbia maji wakazi wa Maroroni kwa siku tatu wakati CCM ilishindwa kwa miaka 50.

“Mnashindwa kuiondoa Gawasa ambayo inachukua pesa zetu bure za maji lakini huduma yenyewe hawatoi maji unapata kwa wiki mara moja ankara inakuwa ya juu tutaweza wapi maisha haya,” walisema wakazi hao.

Mkutano huo ilivunjika huku Katibu mwenezi wa CCM Babati,Adam Ipingika akiwataka wananchi wakaulize maswali yao Chadema na waziri huyo akaondoka na msafara wake akisindikizwa na kelele na kuonyeshwa vidole viwili na baadhi ya wakazi hao.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment