TATIZO la muda mrefu la uhaba wa maji kwa
wakazi wa kijiji cha Galapo Wilayani Babati Mkoani Manyara limesababisha
kuvunjika kwa mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Waziri wa maji Profesa
Jumanne Maghembe baada ya waziri huyo kuwakejeli wapinzani kuwa hawawezi kuwapa
maji wananchi hao.
Hali hiyo ilijitokeza juzi kijijini hapo
ambapo Prof Magembe alifika eneo hilo na kutegemewa na wananchi kuwa atavunja
Mamlaka ya maji safi na maji taka Galapo (Gawasa) wanaodaiwa kuchukua fedha
lakini hawatoi huduma ya maji.
Awali,waziri huyo alizungumza na wakazi hao na
kudai kuwa ni lazima wananchi wachangie huduma ya maji ili mamlaka ziweze
kununua vifaa vinavyohitajika katika kuendesha miradi husika,kwani hiyo ndiyo
sera ya Serikali ya CCM.
“Naagiza kuwa maji yatalipiwa ili huduma iwe
endelevu na agizo hili pia nalielekeza kwa mamlaka za maji za miji midogo yote
nchini iwe Galapo,Dareda,Magugu na Bashnet,” alisema Prof Maghembe.
Hali ya mkutano huo,ilibadilika baada ya
waziri huyo kudai kuwa wapinzani wanakuwa na maneno mengi lakini ukiwaambia
watekeleze jambo lolote wana shindwa na kubaki kuilaumu CCM.
“Hawa wapinzani kama ni matusi wacha
wanitukane tu lakini suala la kuwapa maji eneo hili hawawezi ni kelele tu za
bure nyie endeleeni kuchangia maji mnayotumia kwani ndiyo sera yetu,” alisema
Prof Maghembe.
Kauli hiyo iliamsha nyongo za wakazi hao
zilizolala,kwani baadhi yao walianza kuonyesha vidole viwili hewani na kudai
kuwa wapinzani wataweza kuleta maji
kwani kuna baadhi ya maeneo wameweza.
Baadhi yao walipasa sauti na kudai kuwa
Chadema ina uwezo wa kuleta maji kwani mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki,Joshua
Nassari aliweza kuwachimbia maji wakazi wa Maroroni kwa siku tatu wakati CCM
ilishindwa kwa miaka 50.
“Mnashindwa kuiondoa Gawasa ambayo inachukua
pesa zetu bure za maji lakini huduma yenyewe hawatoi maji unapata kwa wiki mara
moja ankara inakuwa ya juu tutaweza wapi maisha haya,” walisema wakazi hao.
Mkutano huo ilivunjika huku Katibu mwenezi wa
CCM Babati,Adam Ipingika akiwataka wananchi wakaulize maswali yao Chadema na
waziri huyo akaondoka na msafara wake akisindikizwa na kelele na kuonyeshwa
vidole viwili na baadhi ya wakazi hao.
MWISHO.
|