MAMLAKA ya Mji mdogo wa Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imetenga viwanja 500 kwa ajili ya kuwapatia
waathirika wa mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni ili
wajenge nyumba na kuhama mabondeni.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa
Mirerani, Adam Kobelo akizungumza jana alisema waliopatiwa viwanja hivyo
wanapaswa kujenga makazi yao baada ya kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja
baada ya kukabidhiwa viwanja vyao.
Kobelo alisema hawataruhusu wale wote
waliopatiwa viwanja hivyo kuviuza kwani lengo lao ni kuhakikisha waathirika wa
mafuriko wanahama mabondeni na kujenga makazi mapya.
"Tuliona ni busara kuwapa
waathirika wa mafuriko na pia baadhi ya watu waliokuwa wanapangisha kwenye
nyumba hizo ili watu wale wale wasije wakapata tatizo lile lile kwa mwaka
kesho," alisema Kobelo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchumi, Ujenzi na Mazingira wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani, Rajabu Msuya,
alisema suala la kugawa viwanja kwa wahitaji haijawahi kutokea tangu mamlaka
hiyo ianzishwe.
Msuya alisema wamepitia changamoto
nyingi ikiwemo lawama wakati wa zoezi la ugawaji wa viwanja hivyo japo wenyewe
hawana hofu kwani wanafanya kazi ya jamii ambayo halikwepeki kulalamikiwa.
"Niwapongeze wenyeviti wote kwa
kuendesha vizuri zoezi hili vizuri kuanzia Mwenyekiti wa mamlaka Adam Kobelo,
Mwenyekiti wa kamati yetu Joseph Masasi na ofisa mtendaji wa mamlaka Evans
Mbogo walisimama vyema kwenye jambo hili," alisema Msuya.
Mwenyekiti wa mtaa wa Tunduru,
Christopher Chengula alisema wametoa viwanja kwa wananchi wa maeneo yote
yaliyoathirika na watu wenye uhitaji.
Chengula alisema wananchi wa
vitongoji saba vya mji mdogo wa Mirerani, ambao wameathirika na mafuriko na
watu wenye uhitaji maalum wamepatiwa viwanja vya kujenga makazi mapya.
Mmoja kati ya wakazi wa mji mdogo wa
Mirerani, Jacklin Momo aliipongeza serikali kwa kufanikisha zoezi hilo la
ugawaji wa viwanja kwa waathirika wa mafuriko na watu wengine wenye uhitaji.
Momo alisema waathirika waliokumbwa
na mafuriko kwenye maeneo yote ya mji mdogo wa Mirerani wamepatiwa viwanja
vipya hivyo serikali inapaswa kupongezwa kwa jambo hilo.
No comments:
Post a Comment