MBUNGE wa viti maalumu wa Mkoa wa
Manyara (CCM) Ester Alexander Mahawe amezitaka halmashauri Mkoani humo kuhakikisha wanazingatia utoaji
wa mikopo kwa akina mama, vijana na walemavu
haraka iwezekabavyo ili kuyakomboa makundi hayo ambayo yamekuwa yakikumbwa
na changamoto nyingi katika jamii na kubebeshwa majukumu mazito.
Hayo yalibainishwa na Mbunge Mahawe
wakati akizungumza kwenye ziara ya mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti aliyekuwa
ziarani humo kwa siku nne wilayani Babati, kwa ziara ya siku nne baada ya mkuu
huyo kuzindua zahanati ya Madunga na kufuatiwa na mkutano wa hadhara.
Alisema wanawake ndiyo chachu katika kupambana na
umaskini na vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa kadhalika kundi la walemavu wana
michango mikubwa katika familia na Taifa kwa ujumla hivyo ni vema mikopo yao
ikatolewa kwa wakati muafaka ili kuweza kujiendeleza kiuchumi na hatimaye
kuondokana na umaskini.
Mahawe alisema ni vema sasa
halmashauri zikahakikisha na kutambua kuwa mikopo hiyo siyo hisani bali ni kwa
mujibu wa sheria na hivyo inatakiwa
kutolewa kwa wakati ili iweze kusaidia vikundi husika na kuleta tija kwa jamii
husika katika kupambana na umaskini.
"Naomba tambueni kuwa mikopo hii
inatolewa siyo kama hisani kwa wenzetu, bali kwa mujibu na sheria na hivyo katika utoaji mikopo hiyo maafisa maendeleo ya jamii wa
halmashauri wanapaswa kuzingatia makundi yote yanayolengwa ikiwemo
kinamama, vijana na walemavu kama ambavyo serikali imeagiza na siyo
vinginevyo" alisema Mbunge Mahawe.
Mahawe alisema serikali ina nia njema
ya kuona jamii yake inaendelea kiuchumi
kupitia makundi hayo hivyo imeamua kutoa
riba kwenye mikopo hiyo ili waweze
kujiendeleza zaidi na zaidi na kujikuza katika biashara zao, huku lengo la
serikali likiwa ni kuwaondoa katika wimbi la umaskini wananchi wake.
“Katika hili sitaweza kumung'unya
maneno, maafisa maendeleo ya jamii wa
halmashauri zetu wanapaswa kuhakikisha wanatoa elimu ya biashara kwa ufasaa
zaidi kabla ya kutoa mikopo hiyo ili
wanawake waweze kupata elimu hiyo kikamilifu na hatimaye iweze kuwasaidia kina
mama wale , wasije kuitumia kwa starehe ,kununulia vitenge vya wax baadaye
wakashindwa kuirejesha, kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa bado hatujawasaidia wanawake hawa
ambao ndio chachu katika ya maendeleo katika kaya na Taifa kiujumla,"
alisema mbunge Mahawe.
Aliwataka wanawake kuelewa kuwa
wanatakiwa kuwekeza ili waweze kurejesha mikopo kwa wakati kwani wasipofanya
hivyo watawanyima wanawake wenzao fursa, na kuwaonya Wanaume wenye mtindo wa
kuwanyanganya wanawake fedha hizo za mikopo na kuwakwamisha katika biashara.
“Nani hapa ambaye hajui kuwa mwanamke
ndiyo mchumi katika familia, wapo baadhi ya waume zetu wanaodiriki kumnyang’anya
fedha hizo mwanamke, hakika wanaye Mungu
anawaona huo ni ukatili wa kijinsia,
wanawake mnapofanyiwa hivyo
mnapaswa kutoa taarifa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa haraka
iwezekanavyo,” alisema Mahawe.
Aidha katika hatua nyingine Mbunge
huyo alitoa msaada wa mashuka 30 yenye thamani ya zaidi ya sh.600,000 katika
zahanati za Boay, Gijedabong na Madunga
wakati wa ufunguzi wa zahanati hizo
na kuwataka wananchi wa maeneo hayo kuwa waangalifu na kuyatunza majengo
hayo na vifaa ikiwemo dawa ili
kuhakikisha dawa zinazopelekwa na serikali ziweze kusaidia wananchi wa maeneo
hayo.
Alisema katika kuboresha sekta ya afya, Serikali
imeendelea kutoa fedha za kuboresha vituo vyya Afya ili kina mama wajawazito waondokane
na adha ya kuzifuata huduma hizo kwa umbali mrefu na kupunguza vifo kipindi
cha kujifungua.
Hivi karibuni, mbunge Mahawe alitoa msaada wa shuka 20 kwa ajili ya kituo cha Afya cha Mirerani, katika Halmashauri
ya wilaya ya Simanjiro mkoani humo ili
kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha huduma za afya hapa nchini.
No comments:
Post a Comment