MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander
Mnyeti amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Hamis
Malinga kumsimamisha kazi ofisa mtendaji wa Kijiji cha Ayasanda anayetuhumiwa
kufuja sh13 milioni fedha za michango ya wananchi ya mradi wa zahanati.
Mnyeti akizungumza kijijini
hapo, amemuagiza Malinga kuandika barua kwa mkuu wa chuo hicho ili mtendaji
huyo John Simon ambaye hivi sasa anasoma chuo cha uongozi Hombolo jijini Dodoma
arudi Babati.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo
mara baada ya mmoja kati ya wakazi wa kijiji hicho John Lorry kulalamikia
kufujwa kwa fedha za wananchi walizochanga ili kufanikisha mradi huo wa
zahanati.
Lorry alisema wananchi wa eneo hilo
walichanga fedha zao kwa ajili ya kuufanikisha ujenzi wa zahanati yao kutokana
na kutembelea umbali mrefu kufuata huduma ya afya lakini wakakwamishwa na
ufujaji wa fedha hizo.
"Tulitegemea huyo mtendaji wa
kijiji achukuliwe hatua kali kwa kufuja fedha zetu lakini wanabebana tuu hapa
kwani alikuja akapiga siasa bila kurudisha michango ya wananchi ya ujenzi wa
zahanati," alisema Lorry.
Akijibu kuhusu hilo mkuu huyo wa mkoa
aliagiza mtendaji huyo wa kijiji kurudishwa mara moja kwenye eneo hilo ili
ajibu tuhuma hizo na endapo atashindwa kuzilipa fedha hizo sh13milioni
afikishwe mahakamani.
"Watendaji kama hawa ndiyo
wanasababaisha wananchi wasichangie miradi mingine ya maendeleo kwani wanahofia
fedha zao kuliwa badala ya kupelekwa kwenye lengo husika kama alivyofanya huyo mtendaji,"
alisema Mnyeti.
Aliwaagiza maofisa watendaji wa
vijiji na kata za mkoa huo kuhakikisha wanasimamia vyema michango ya wananchi
kwani atawachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kufuja fedha za
maendeleo.
"Mtumishi yeyote atakayefuja
fedha Manyara na kuomba uhamisho akahamia mkoa wowote iwe Mwanza au wapi
tutaandika barua kule utumishi ili arudishwe Manyara kisha tutamfukuzia kazi
hapa hapa Manyara hawezi kukwepa hilo," alisema Mnyeti.
Hata hivyo, Malinga aliahidi
kutekeleza agizo hilo kwa kuhakikisha mtendaji huyo wa kijiji anarejeshwa
kijijini hapo kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Alisema awali, alimuagiza mkaguzi wa
ndani wa halmashauri ya wilaya hiyo, kukagua hesabu za mradi huo na kusoma
taarifa yake mbele ya mkutano mkuu wa kijiji ambapo mtendaji huyo alijitetea
kuwa hakufuja fedha hizo.
No comments:
Post a Comment