WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amempongeza Mbunge wa viti maalum Mkoa wa
Manyara, Martha Umbullah (CCM) kwa kuwa mdau mkubwa wa kuwawezesha wanawake wa
mkoa huo kiuchumi, kwani ameacha alama isiyofutika kwa wanawake wa mkoa huo.
Waziri Mwalimu aliyazungumza mjini
Mbulu Mkoani Manyara, kwenye maazimisho ya miaka 25 ya shirika lisilo la
kiserikali linaloshughulikia utoaji wa mikopo midogo midogo na mafunzo ya
ujasiriamali kwa wanawake (WEDAC).
Waziri Mwalimu alisema anatambua
mchango mkubwa unaotolewa na Mbunge Umbullah kwa jitihada zake ambazo
ameendelea kuchukua kupitia shirika la WEDAC ambapo wanaunga mkono jitihada za
serikali katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.
"Hongera sana mh.Umbullah wewe
ni jembe na mimi naomba niwaambie sisi bungeni tunamtegemea sana, tunamtumainia
sana, ni mama anayejitambua mwenye uchungu kabisa wa maendeleo ya wanawake wa
Manyara lakini na maendeleo ya wanawake wa Tanzania, kwa hivyo naamini na nyie
mtaendelea kushirikiana na serikali katika kufikia utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya CCM,” alisema Waziri Ummy.
Alisema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya
kufikiwa kwa usawa wa jinsia uwezeshaji wa wanawake ikiwemo kwa wanawake
wa vijijini na ndio maana wakati serikali ya awamu ya tano chini ya Rais
Magufuli ilipoingia madarakani ilifanya mambo makubwa mawili kwa upande wa
wanawake kuanzisha majukwaa ya kiuchumi ya wanawake, ambapo kwa mkoa lipo, na
kwa Mbulu nalo pia lipo la kuwezesha wanawake kiuchumi ambalo lilianzishwa na
makamu wa raisi Mama Samia Suluhu Hasan.
Alisema yale majukwaa yatasaidia
wanawake wajasiriamali kukutana na kuzungumzia changamoto mbalimbali
zinazowakabili, hivyo jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi ndilo jukwaa rasmi la kiserikali, hivyo wafanye
uhamasishaji wa kuwaungunisha wanawake wote kujiunge kwenye jukwaa hilo.
"Lakini pia tutaendelea na
jitihada za kusimamia na kuratibu
utekelezaji wa mfuko wa maendeleo ya wanawake ambao unatoa mikopo yenye
masharti nafuu kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogo ili kuanzisha na kuendeleza biashara,
viwanda vidogo, kilimo na shughuli zingine za kiuchumi," alisema Waziri
Ummy.
Aidha kupitia hilo Halmashauri
zimetakiwa kuchangia asilimia 4 kupitia
mapato yao ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha wanawake, asilimia 4 vijana
na asilimia 2 kwa ajili ya kuchangia
mahitaji ya watu wenye ulemavu.
"Nashukuru kwa kupeleka fedha
kwenye vikundi vya wanawake vyenye
jumla. ya sh.mil.21, 700,000 kutoka halamshauri ya wilaya ya mbulu lakini pia
halmashauri ya mji wa mbulu," alisema Waziri Mwalimu.
Mbunge wa viti maalum mkoani
Manyara Martha Umbullah (CCM) alimshukuru
Waziri Ummy Mwalimu kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla ya maadhimisho
ya miaka 25 ya shirika linaloshughulikia utoaji wa mikopo kidogo kidogo na
mafunzo ya ujasiriamali (WEDAC).
Alisema WEDAC ipo katika
misingi ya utekelezaji wa ilani
ya uchaguzi wa CCM mwaka 2005 wakati
alipoomba ridhaa ya kuongoza wanawake wa mkoa huo, aliwaambia wanawake kuwa
yeye ni mtaalam wa kuomba fedha kwa
wafadhili kwa ajili ya kukopeshana na
kuinua uchumi wa wanawake, waliokuwepo kwa wakati ule wanalijua hilo.
Umbullah alisema kupitia mikopo hiyo
yeye ameweka alama ya kudumu kwa kuwa hata yeye asipokuea mbunge, taasisi hiyo
itaendelea kuwanufaisha wanawake wa mkoa huo iwapo wataendelea kuwa waaminifu
katika urejeshwaji wa mikopo hiyo.
"Waliokuwepo kipindi kile cha
mwaka 2005 wakati wa kuomba ridhaa ya kuwa mbunge kwenye mkoa wangu, nilisema
kuwa mimi niliwaambia akina mama kuwa mimi ni mtaalam kwa kuomba fedha kwa wafadhili kwa hivyo nitawatafutia fursa
kwa wafadhili ili akina mama waendelea kiuchumi," alisema Umbullah.
Alisema kuna wanawake walianza
kukopeshwa kwa sh.200,000 tu, lakini hadi hivi sasa wamefikia kukopa
sh.mil.5,000,000, na wameweza kupata mafanikio mbalimbali yaliyowawezesha
kiuchumi katika nyanja mbalimbali za kuwakomboa katika umaskini.
No comments:
Post a Comment