Saturday, 9 June 2018

DC MOFUGA AANZISHA KAMPENI YA VYETI KWA MANUFAA YA WANANCHI MBULU

 Dc Mbulu aanzisha kampeni ya vyeti vya kuzaliwa, vifo na ndoa kwa manufa ya wananchi.

Mkuu wa wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara Chelestino Simbalimile Mofuga ameanzisha kampeni ya wananchi wilayani Mbulu ya vyeti vya kuzaliwa, vifo na ndoa.

kampeni hiyo imezinduliwa katika kata tatu ikiwemo kata ya Ayamaami, Uhuru na kata ya Imboru.

Mofuga amesema ni vyema kila mwananchi kuwa na cheti cha kuzaliwa ili kuepuka usumbufu na kutambulika katika eneo lake  kwani mwananchi akiwa na cheti cha kuzaliwa anakuwa salama na akihitaji huduma ni rahisi kuhudumiwa katika eneo lake.

pamoja na hilo amesema vyeti vya ndoa na vifo ni muhimu sana kwa mwananchi ili inapotokea mmoja amefariki itamsaidia ailiyebaki katika kusimamia mirathi bila kuingiliwa na mtu yeyote wa upande mwingine.


Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Mbulu amesema kwamba wilaya ya Mbulu inakabiliwa na  changamoto ya matumizi ya risiti na kuwataka wananchi kutoanunua bidhaa katika maduka ambayo hayatoi risiti ili kuepuka usumbufu wa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria kwani mwananchi akikamatwa ana bidhaa aliyonunua bila risiti atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

katika maeneo hayo aliyoyapitia nakufanya mkutano wa hadhara mkuu wa wilaya amewataka wananchi kutopika wala kunywa pombe haramu aina ya gongo na pia kutouza pombe kabla ya saa tisa alasiri.

Kwa kata ya Uhuru ameagiza wenyeviti wa mitaa kusimamia wananchi wasinywe pombe kabla ya saa tisa vinginevyo watawajibika wao wenyewe kwani mtaa wa Uhuru unasifika sana kwa unywaji wa pombe badala ya kufanya kazi.

Katika kata tatu alizoanza nazo tarehe 8.06.2018 katika kata tatu ambazo ni kata ya Ayamaami,uhuru na Imboru kata ya Imboru mahudhurio hayakuwa mazuri na ameagiza wenyeviti wa mitaa siku  ya tarehe 11.06.2018 kufika katika ofisi yake wakiwa na maelezo ya kutosha ya kwanini wananchi hawajajitokeza.

Pamoja na maelezo hayo amewataka wenyeviti waende na tozo ya shilingi 5,000/ kwa kila kichwa kwa wale wote  ambao hawahudhuria kikao chake cha kiserikali yenye lengo la kutoa maagizo muhimu.

Amesema wananchi wote ambao hawajashiriki mkutano wake wanafikia 1004  na kwa tozo hizo watakazotoa watafikisha million tano ambayo imepitishwa kupelekwa kwenye shule ya msingi Isale kwa ajili ya kupeleka maji.

Kauli mbiu cheti cha kuzaliwa nyumba kwa nyumba


Friday, 8 June 2018

TUNAMPOKEA MBUNGE FLATEI MASSAY

 Wananchi waJimbo la Mbulu Vijijini Mkoani Manyara, wakimpokea mbunge wa jimbo hilo Flatei Gregory Massay alipowatembelea kuzungumza nao na kusikiliza changamoto na kero zao.

WAZIRI UMMY MWALIMU AMFAGILIA MBUNGE UMBULLAH

 WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amempongeza Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara, Martha Umbullah (CCM) kwa kuwa mdau mkubwa wa kuwawezesha wanawake wa mkoa huo kiuchumi, kwani ameacha alama isiyofutika kwa wanawake wa mkoa huo.

Waziri Mwalimu aliyazungumza mjini Mbulu Mkoani Manyara, kwenye maazimisho ya miaka 25 ya shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia utoaji wa mikopo midogo midogo na mafunzo ya ujasiriamali  kwa wanawake (WEDAC).
Waziri Mwalimu alisema anatambua mchango mkubwa unaotolewa na Mbunge Umbullah kwa jitihada zake ambazo ameendelea kuchukua kupitia shirika la WEDAC ambapo wanaunga mkono jitihada za serikali katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.

"Hongera sana mh.Umbullah wewe ni jembe na mimi naomba niwaambie sisi bungeni tunamtegemea sana, tunamtumainia sana, ni mama anayejitambua mwenye uchungu kabisa wa maendeleo ya wanawake wa Manyara lakini na maendeleo ya wanawake wa Tanzania, kwa hivyo naamini na nyie mtaendelea kushirikiana na serikali katika kufikia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM,” alisema Waziri Ummy.
 Alisema serikali itaendelea  kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kufikiwa  kwa usawa wa jinsia  uwezeshaji wa wanawake ikiwemo kwa wanawake wa vijijini na ndio maana wakati serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ilipoingia madarakani ilifanya mambo makubwa mawili kwa upande wa wanawake kuanzisha majukwaa ya kiuchumi ya wanawake, ambapo kwa mkoa lipo, na kwa Mbulu nalo pia lipo la kuwezesha wanawake kiuchumi ambalo lilianzishwa na makamu wa raisi Mama Samia Suluhu Hasan.

Alisema yale majukwaa yatasaidia wanawake wajasiriamali kukutana na kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili, hivyo jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi ndilo  jukwaa rasmi la kiserikali, hivyo wafanye uhamasishaji wa kuwaungunisha wanawake wote kujiunge kwenye jukwaa hilo.

"Lakini pia tutaendelea na jitihada za kusimamia na kuratibu  utekelezaji wa mfuko wa maendeleo ya wanawake ambao unatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali  wadogo ili kuanzisha na kuendeleza biashara, viwanda vidogo, kilimo na shughuli zingine za kiuchumi," alisema Waziri Ummy.

Aidha kupitia hilo Halmashauri zimetakiwa kuchangia asilimia 4  kupitia mapato yao ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha wanawake, asilimia 4 vijana na  asilimia 2 kwa ajili ya kuchangia mahitaji ya watu wenye ulemavu.

"Nashukuru kwa kupeleka fedha kwenye vikundi vya wanawake  vyenye jumla. ya sh.mil.21, 700,000 kutoka halamshauri ya wilaya ya mbulu lakini pia halmashauri ya mji wa mbulu," alisema Waziri Mwalimu.

Mbunge wa viti maalum mkoani Manyara  Martha Umbullah (CCM) alimshukuru Waziri Ummy Mwalimu kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya shirika linaloshughulikia utoaji wa mikopo kidogo kidogo na mafunzo  ya ujasiriamali  (WEDAC).

Alisema WEDAC ipo  katika  misingi  ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM  mwaka 2005 wakati alipoomba ridhaa ya kuongoza wanawake wa mkoa huo, aliwaambia wanawake kuwa yeye ni mtaalam wa kuomba fedha  kwa wafadhili  kwa ajili ya kukopeshana na kuinua uchumi wa wanawake, waliokuwepo kwa wakati ule wanalijua hilo.

Umbullah alisema kupitia mikopo hiyo yeye ameweka alama ya kudumu kwa kuwa hata yeye asipokuea mbunge, taasisi hiyo itaendelea kuwanufaisha wanawake wa mkoa huo iwapo wataendelea kuwa waaminifu katika urejeshwaji wa mikopo hiyo.

"Waliokuwepo kipindi kile cha mwaka 2005 wakati wa kuomba ridhaa ya kuwa mbunge kwenye mkoa wangu, nilisema kuwa mimi niliwaambia akina mama kuwa mimi ni mtaalam kwa kuomba fedha  kwa wafadhili kwa hivyo nitawatafutia  fursa  kwa wafadhili ili akina mama waendelea kiuchumi," alisema Umbullah.

Alisema kuna wanawake walianza kukopeshwa kwa sh.200,000 tu, lakini hadi hivi sasa wamefikia kukopa sh.mil.5,000,000, na wameweza kupata mafanikio mbalimbali yaliyowawezesha kiuchumi katika nyanja mbalimbali za kuwakomboa katika umaskini.

MBUNGE MAHAWE AZITAKA HALMASHAURI KUTOA MIKOPO KWA WAKATI

 MBUNGE wa viti maalumu wa Mkoa wa Manyara (CCM) Ester Alexander Mahawe amezitaka halmashauri  Mkoani humo kuhakikisha wanazingatia utoaji wa mikopo kwa akina mama, vijana na walemavu  haraka iwezekabavyo ili kuyakomboa makundi hayo ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto nyingi katika jamii na kubebeshwa majukumu mazito.

Hayo yalibainishwa na Mbunge Mahawe wakati akizungumza kwenye ziara ya mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti aliyekuwa ziarani humo kwa siku nne wilayani Babati, kwa ziara ya siku nne baada ya mkuu huyo kuzindua zahanati ya Madunga na kufuatiwa na mkutano wa hadhara.

Alisema  wanawake ndiyo chachu katika kupambana na umaskini na vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa kadhalika kundi la walemavu wana michango mikubwa katika familia na Taifa kwa ujumla hivyo ni vema mikopo yao ikatolewa kwa wakati muafaka ili kuweza kujiendeleza kiuchumi na hatimaye kuondokana na umaskini.

Mahawe alisema ni vema sasa halmashauri zikahakikisha na kutambua kuwa mikopo hiyo siyo hisani bali ni kwa mujibu wa sheria na hivyo  inatakiwa kutolewa kwa wakati ili iweze kusaidia vikundi husika na kuleta tija kwa jamii husika katika kupambana na umaskini.

"Naomba tambueni kuwa mikopo hii inatolewa siyo kama hisani kwa wenzetu, bali kwa mujibu na sheria na hivyo  katika utoaji mikopo  hiyo maafisa maendeleo ya jamii wa halmashauri wanapaswa kuzingatia makundi yote yanayolengwa  ikiwemo  kinamama, vijana na walemavu kama ambavyo serikali imeagiza na siyo vinginevyo" alisema Mbunge Mahawe.

Mahawe alisema serikali ina nia njema ya  kuona jamii yake inaendelea kiuchumi kupitia makundi hayo hivyo  imeamua kutoa riba kwenye mikopo  hiyo ili waweze kujiendeleza zaidi na zaidi na kujikuza katika biashara zao, huku lengo la serikali likiwa ni kuwaondoa katika wimbi la umaskini wananchi wake.

“Katika hili sitaweza kumung'unya maneno, maafisa maendeleo ya jamii  wa halmashauri zetu wanapaswa kuhakikisha wanatoa elimu ya biashara kwa ufasaa zaidi  kabla ya kutoa mikopo hiyo ili wanawake waweze kupata elimu hiyo kikamilifu na hatimaye iweze kuwasaidia kina mama wale , wasije kuitumia kwa starehe ,kununulia vitenge vya wax baadaye wakashindwa kuirejesha, kwani kwa kufanya hivyo   tutakuwa bado hatujawasaidia wanawake hawa ambao ndio chachu katika ya maendeleo katika kaya na Taifa kiujumla," alisema mbunge Mahawe.

Aliwataka wanawake kuelewa kuwa wanatakiwa kuwekeza ili waweze kurejesha mikopo kwa wakati kwani wasipofanya hivyo watawanyima wanawake wenzao fursa, na kuwaonya Wanaume wenye mtindo wa kuwanyanganya wanawake fedha hizo za mikopo na kuwakwamisha katika biashara.

“Nani hapa ambaye hajui kuwa mwanamke ndiyo mchumi katika familia, wapo baadhi ya waume zetu wanaodiriki kumnyang’anya fedha hizo  mwanamke, hakika wanaye Mungu anawaona huo ni ukatili wa kijinsia,  wanawake mnapofanyiwa hivyo  mnapaswa kutoa taarifa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa haraka iwezekanavyo,” alisema Mahawe.

Aidha katika hatua nyingine Mbunge huyo alitoa msaada wa mashuka 30 yenye thamani ya zaidi ya sh.600,000 katika zahanati za Boay, Gijedabong na Madunga  wakati wa ufunguzi wa zahanati hizo  na kuwataka wananchi wa maeneo hayo kuwa waangalifu na kuyatunza majengo hayo na vifaa ikiwemo dawa  ili kuhakikisha dawa zinazopelekwa na serikali ziweze kusaidia wananchi wa maeneo hayo.

Alisema  katika kuboresha sekta ya afya, Serikali imeendelea kutoa fedha za kuboresha vituo vyya Afya ili kina mama wajawazito waondokane na adha ya kuzifuata huduma hizo kwa umbali mrefu na kupunguza vifo kipindi cha  kujifungua.

Hivi karibuni, mbunge Mahawe alitoa msaada wa shuka 20 kwa ajili ya kituo cha Afya cha Mirerani, katika Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoani humo  ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha huduma za afya hapa nchini.

VEO ASIMAMISHWA KAZI KWA KUFUJA FEDHA ZA MRADI WA MAENDELEO

 MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Hamis Malinga kumsimamisha kazi ofisa mtendaji wa Kijiji cha Ayasanda anayetuhumiwa kufuja sh13 milioni fedha za michango ya wananchi ya mradi wa zahanati.

Mnyeti akizungumza kijijini hapo, amemuagiza Malinga kuandika barua kwa mkuu wa chuo hicho ili mtendaji huyo John Simon ambaye hivi sasa anasoma chuo cha uongozi Hombolo jijini Dodoma arudi Babati.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo mara baada ya mmoja kati ya wakazi wa kijiji hicho John Lorry kulalamikia kufujwa kwa fedha za wananchi walizochanga ili kufanikisha mradi huo wa zahanati.


Lorry alisema wananchi wa eneo hilo walichanga fedha zao kwa ajili ya kuufanikisha ujenzi wa zahanati yao kutokana na kutembelea umbali mrefu kufuata huduma ya afya lakini wakakwamishwa na ufujaji wa fedha hizo.

"Tulitegemea huyo mtendaji wa kijiji achukuliwe hatua kali kwa kufuja fedha zetu lakini wanabebana tuu hapa kwani alikuja akapiga siasa bila kurudisha michango ya wananchi ya ujenzi wa zahanati," alisema Lorry.

Akijibu kuhusu hilo mkuu huyo wa mkoa aliagiza mtendaji huyo wa kijiji kurudishwa mara moja kwenye eneo hilo ili ajibu tuhuma hizo na endapo atashindwa kuzilipa fedha hizo sh13milioni afikishwe mahakamani.

"Watendaji kama hawa ndiyo wanasababaisha wananchi wasichangie miradi mingine ya maendeleo kwani wanahofia fedha zao kuliwa badala ya kupelekwa kwenye lengo husika kama alivyofanya huyo mtendaji," alisema Mnyeti.

Aliwaagiza maofisa watendaji wa vijiji na kata za mkoa huo kuhakikisha wanasimamia vyema michango ya wananchi kwani atawachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kufuja fedha za maendeleo.

"Mtumishi yeyote atakayefuja fedha Manyara na kuomba uhamisho akahamia mkoa wowote iwe Mwanza au wapi tutaandika barua kule utumishi ili arudishwe Manyara kisha tutamfukuzia kazi hapa hapa Manyara hawezi kukwepa hilo," alisema Mnyeti.

Hata hivyo, Malinga aliahidi kutekeleza agizo hilo kwa kuhakikisha mtendaji huyo wa kijiji anarejeshwa kijijini hapo kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.

Alisema awali, alimuagiza mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya wilaya hiyo, kukagua hesabu za mradi huo na kusoma taarifa yake mbele ya mkutano mkuu wa kijiji ambapo mtendaji huyo alijitetea kuwa hakufuja fedha hizo.


MAMLAKA YA MJI MDOGO WA MIRERANI YAGAWA VIWANJA

 MAMLAKA ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imetenga viwanja 500 kwa ajili ya kuwapatia waathirika wa mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni ili wajenge nyumba na kuhama mabondeni.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo akizungumza jana alisema waliopatiwa viwanja hivyo wanapaswa kujenga makazi yao baada ya kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja baada ya kukabidhiwa viwanja vyao.

Kobelo alisema hawataruhusu wale wote waliopatiwa viwanja hivyo kuviuza kwani lengo lao ni kuhakikisha waathirika wa mafuriko wanahama mabondeni na kujenga makazi mapya.

"Tuliona ni busara kuwapa waathirika wa mafuriko na pia baadhi ya watu waliokuwa wanapangisha kwenye nyumba hizo ili watu wale wale wasije wakapata tatizo lile lile kwa mwaka kesho," alisema Kobelo.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani, Rajabu Msuya, alisema suala la kugawa viwanja kwa wahitaji haijawahi kutokea tangu mamlaka hiyo ianzishwe.

Msuya alisema wamepitia changamoto nyingi ikiwemo lawama wakati wa zoezi la ugawaji wa viwanja hivyo japo wenyewe hawana hofu kwani wanafanya kazi ya jamii ambayo halikwepeki kulalamikiwa.

"Niwapongeze wenyeviti wote kwa kuendesha vizuri zoezi hili vizuri kuanzia Mwenyekiti wa mamlaka Adam Kobelo, Mwenyekiti wa kamati yetu Joseph Masasi na ofisa mtendaji wa mamlaka Evans Mbogo walisimama vyema kwenye jambo hili," alisema Msuya.

Mwenyekiti wa mtaa wa Tunduru, Christopher Chengula alisema wametoa viwanja kwa wananchi wa maeneo yote yaliyoathirika na watu wenye uhitaji.

Chengula alisema wananchi wa vitongoji saba vya mji mdogo wa Mirerani, ambao wameathirika na mafuriko na watu wenye uhitaji maalum wamepatiwa viwanja vya kujenga makazi mapya.

Mmoja kati ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, Jacklin Momo aliipongeza serikali kwa kufanikisha zoezi hilo la ugawaji wa viwanja kwa waathirika wa mafuriko na watu wengine wenye uhitaji.

Momo alisema waathirika waliokumbwa na mafuriko kwenye maeneo yote ya mji mdogo wa Mirerani wamepatiwa viwanja vipya hivyo serikali inapaswa kupongezwa kwa jambo hilo.


MAMBO YA FUTARI

Mambo ya futari hayoooo, mkazi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Muhsin Issa akinunua boga kwa ajili ya kufuturu kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, boga hilo huuzwa kwa shilingi elfu 4.