Mkurugenzi Mtendaji mpya
wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Yefred Myenzi amesema
atahakikisha anakabiliana na migogoro ya ardhi kwa kusimamia sheria za ardhi na
kuimarisha mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata.
Myenzi akizungumza wakati akisoma salamu zake kwenye kikao cha robo ya nne cha baraza la
madiwani wa halmashauri hiyo alisema atahakikisha mabaraza ya ardhi ya vijiji
na kata yanaundwa kwenye sehemu ambapo hayapo.
Alisema karibu kila
kijiji cha wilaya hiyo kina migogoro ya ardhi yenye sura nyingi ukiacha ile
inayotokana na kukosa uelewa na baadhi ya maeneo ambayo migogoro yake inahusu
uvamizi na kuibukua kwa soko holela la kuuza ardhi.
“Ipo migogoro yenye
sura ya kisiasa na mingine ya kukosa uelewa ila migogoro mingi inachochewa na
uhaba wa rasilimali hasa malisho na maji nyakati za kiangazi na nitapambana
nayo ili tuhakikishe tunaimaliza,” alisema Myenzi.
Alisema anaomba
ushirikiano wa makundi yote ya kijamii hasa wafugaji na wakulima, mamlaka ya
hifadhi, taasisi za umma na binafsi katika kupanga miji ya Orkesumet, Mirerani
na maeneo mengine ya biashara yanayokua kwa kasi.
Alisema moja ya
dhamana kubwa aliyopewa kwa kazi yake ni kuhakikisha anasimamia upatikanaji wa
halali, mgawanyo wa haki na matumizi sahihi ya rasilimali za umma ili kuwezesha
upatikanaji huduma za msingi na maendeleo.
“Wenzetu
waliotutangulia walifanya walichoweza kwa nafasi yao na sisi tumepewa fursa hii
tuitumie kuandika historia kwa vizazi vijavyo ili tuache urathi usiofutika kwa
maisha ya wananchi wa simanjiro,” alisema Myenzi.
Alisema yote hayo
yatawezekana ili mradi kuwepo na msukumo wa pamoja baina ya uongozi na wananchi
na utekelezaji wa masuala hayo katka ngazi ya halmashauri na yapo maagizo ya
kitaifa ambayo hayana budi kutiliwa mkazo.
Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck alisema japokuwa Myenzi bado hajamaliza
hata mwezi mmoja tangu aanze kazi kwenye eneo hilo lakini kwa muda mfupi
waliokuwa nao anaonyesha ataisaidia wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment