Madini ya Tanzanite yenye
thamani ya dola 4.3 milioni za Marekani sawa na sh7.4 bilioni yameuzwa kwenye
mnada wa madini hayo uliofanyika kwa muda wa siku nne jijini Arusha, huku
Serikali ikipata mrabaha wa sh378 milioni.
Katika mnada huo,
kampuni ya TanzaniteOne na Shirika la madini (Stamico) waliongoza kwa kuuza
madini ya dola milioni 3.3 sawa na sh7.3 bilioni na serikali ikapata mrabaha wa
sh367 milioni na kampuni ya Franone iliuza dola laki 1 sawa na sh235 milioni na
serikali ikapata mrabaha wa10 milioni.
Mkurugenzi wa
uthaminishaji wa madini ya almasi na vito wa Wizara ya Nishati na Madini,
Archard Kalugendo aliyasema hayo jijini Arusha, wakati Mkuu wa mkoa wa Manyara,
Dk Joel Bendera akifunga mnada wa madini ya Tanzanite.
Kalugendo alisema wachimbaji
na wanunuzi walioshiriki mnada huo ni makampuni 37 na wachimbaji watano
walijitokeza ni TanzaniteOne na Stamico, Tanzanite Africa/J.S Magezi, Chusa
Mining, Kurian Laizer na Franone Gems.
Alisema makampuni yanayonunua
na kuuza madini ndani na nje ya nchi yalishiriki mnada huo wenye lengo la
kuhakikisha bei ya madini ya Tanzanite ambayo ilikuwa imeshuka inapanda na
kuweka ushindani kwa njia ya minada.
Mkuu wa mkoa wa
Manyara Dk Joel Bendera alisema madini ya Tanzanite yanapatikana eneo moja la
Mirerani wilayani Simanjiro kwa hapa duniani hivyo serikali itaendelea
kudumisha ulinzi na usalama kwa wachimbaji wa madini.
Dk Bendera alisema
kwa mnada huo bei ya Tanzanite itauzwa inavyostahili pia serikali ya wilaya ya
Simanjiro itaweza kukusanya mapato yake ya kodi za huduma kwa urahisi zaidi na hivyo
kutoa huduma za jamii kwa ufanisi zaidi.
“Natoa wito kwa
wachimbaji wote wa madini ya Tanzanite kujitokeza zaidi kwenye mnada ujao kwani
huu kati ya migodi zaidi ya 180 iliyopo Mirerani ni wachimbaji watano pekee
walioshiki katika mnada huu,” alisema Dk Bendera.
Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini Profesa James Mdoe kupitia mnada huo mapato ya nchi
yataongezeka kupitia madini ya Tanzanite na serikali itakusanya mapato yake kwa
urahisi zaidi kwani mnada unafanyika eneo moja.
Profesa Mdoe alisema
kwa sababu mnada huo ni wa mara ya kwanza zipo changamoto zilizojitokeza kwani
ni muda mfupu wa maandalizi ulikuwepo, ila serikali itendelea kuboresha minada
ijayo ili wanufaike na madini ya Tanzanite.
“Kwa njia hii ya mnada
huu pia tunakabiliana na suala la utoroshaji wa madini ya Tanzanite kwenda nchi
za jirani kwani wanunuzi watapata fursa ya kufika kununua wenyewe kuliko
kutorosha,” alisema Profesa Mdoe.
No comments:
Post a Comment