Mkuu wa Mkoa wa
Manyara, Dk Joel Bendera amewaagiza viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Babati
kuhakikisha hadi Desemba mwaka huu kaya 40,642 zinajiunga na mfuko wa afya ya
jamii ulioboreshwa (CHF) hivyo kufikia asilimia 50 ya kaya za wilaya hiyo.
Dk Bendera
amesema wilaya hiyo ina kaya 81,284 hivyo viongozi wa wilaya hiyo wahakikishe
hadi mwezi Desemba wawe wamefanikisha nusu ya kaya zijiunge na mfuko huo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema viongozi
wote wa eneo hilo wanapaswa kuhakikisha jamii inajiunga na mfuko huo kwani ni
ukombozi wao kwenye sekta ya afya na siku wakistaafu wananchi watawakumbuka kwa
kusababisha mabadiliko ya huduma hizo.
“Naibu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto,
Dk Hamis Kigwangalla alitoa agizo kwa mkoa wa Manyara kuhakikisha baada ya
miezi sita ijayo tufikie asilimia 50 ya kaya zote kujiunga na CHF iliyoboreshwa,”
ameeleza.
Malinga amesema
kupitia timu waliyonayo kuanzia ngazi ya vijiji, kata na tarafa, watatimiza
majukumu yao kwa kupeana mrejesho kila mwezi ili kutambua wamefikia hatua gani
na wanatarajia hadi mwezi Desemba watafanikisha.
Meneja wa mfuko
wa Taifa wa bima ya afya nchini (NHIF) mkoani Manyara, Isaya Shekifu amesema mpango wa CHF ulioboreshwa utawawezesha kila kaya ya watu
sita baba, mama na watoto wanne ambao hawajafikisha miaka 18 kupata matibabu
kwa gharama ya sh30,000 katika mwaka mzima.
Shekifu ameeleza kuwa bima ya afya ni muhimu
kwa sababu siyo kila mtu anapopata ugonjwa ana uwezo wa kugharamia matibabu na
nchi zilizoendelea zimefanikiwa kupunguza vifo visivyo na lazima kwa
kuhakikisha watu wanajiunga na mfuko.
“Katika CHF ya zamani huduma za nje tu
ndizo zilizotolewa, hii iliyoboreshwa huduma ya magonjwa ya nje, kulazwa,
upasuaji na vipimo ikiwemo x- ray zinatolewa kwa wanachama waliojiunga bila
kulipia,” amesema Shekifu.
No comments:
Post a Comment