Sunday, 13 September 2015

GEKUL AZINDUA KAMPENI YAKE JIMBO LA BABATI MJINI



Mgombea ubunge  Jimbo la Babati Mjini kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Pauline Gekul ataboresha huduma za jamii na kuwatetea wananchi katika vyombo vya maamuzi, pindi akichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Akizungumza mjini Babati kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho, Gekul alisema endapo atapewa ridhaa na wananchi atadhibiti wizi uliokithiri kwenye halmashauri na kuboresha huduma katika sekta zote.
Alisema akipewa ridhaa hiyo atasimimia ulipwaji wa madai ya watumishi kwa wakati na hasa walimu, madaktari, wauguzi na polisi na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifundishia katika shule za msingi na sekondari, uanzishwaji wa madarasa ya awali katika shule za msingi na ujenzi wa mabweni katika shule za kata.

“Nitajenga  wodi mpya za wazazi hospitali ya Mrara na kupigania vifaa tiba katika hospitali na zahanati, kuanzishwa na kuboreshwa kwa huduma za masoko madogo madogo na kuwaunganisha vijana na  fursa za ajira na kujiajiri wenyewe,” alisema Gekul.

Alisema ataendelea kupigania vifaa tiba vipatikane katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, kuanzisha na kuboresha huduma za masoko madogo madogo katika mitaa yetu, kuwaunganisha vijana na fursa za ajira na kujiajiri wenyewe.

Pia, mgombea huyo aliibua ufisadi wa kutisha  unaofanywa katika halmashauri hiyo huku akishirikiana na wafuasi wake kusoma kitabu cha bajeti na kuonyesha namna ambavyo madiwani walivyotumia fedha za walipakodi.

 “Ninaomba mnitoe kuwa msaidizi mnikabidhi jimbo ili niweze kuwatumikia kikamilifu kama nilikua nafanya nikiwa viti maalum na sikuwa na fungu nikipewa ndiyo nitashindwa jamani naomba mniamini wana Babati,” alisema  Gekul.

Nao, baadhi ya wananchi wa eneo hilo, Restituta Martin, Mussa Hassan na Michael Boay walisema huu ni wakati kwa wananchi wa mji huo kumchagua Gekul ambaye amekuwa akiwatetea wananchi wanyonge hasa migogoro yao. 

1 comment:

  1. hatimaye wananchi wa babati mjini gave u what u want. proud to be your constituent.

    ReplyDelete