Wafugaji wa jamii ya wairaq na wadatoga wa
Bonde la Yaeda Chini, Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, waliokuwa na mgogoro wa
muda mrefu wa eneo la malisho, wamechagua watu 40 watakaosuluhisha ugomvi wao.
Watu hao 40 wamechaguliwa ili kutatua mgogoro
huo, baada ya Mkuu wa wilaya hiyo, Anatory Choya kuagiza wafanye hivyo na
akawapa muda wa wiki mbili wawe wamekutana na kusuluhishana na atawatembelea
tena Machi 18.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Zacharia Paul Isaay alisema kupitia vikao hivyo mauaji, vurugu na migogoro
ya mara kwa mara itamalizika na kufanya jamii ya eneo hilo kuishi kwa amani
kama awali.
“Mnatakiwa muachane na vurugu hizi ambazo
hazina sababu za msingi, ninyi mmekuwa kama ndugu hivi sasa, kwani kuna wairaq
wamewaoa wadatoga na kati yenu hapa kuna wadatoga wamewaoa wairaq,” alisema Isaay.
Mgogoro wa Bonde la Yaeda chini umekuwa ukitokea
mara kwa mara na hadi hivi sasa mauaji ya watu wanne yameshatokea, ambapo hivi
karibuni mfugaji wa jamii ya kiiraqw, Moshi Masabeda (47) aliuawa kwa kuchinjwa
kama kuku.
Akizungumza na jamii hizo, Choya aliagiza ili kumaliza mgogoro huo, inatakiwa wajadili
kukomesha mauaji yanayotokea eneo hilo, kupiga vita wizi wa mifugo na namna ya
kupanga matumizi bora ya ardhi.
Pia, aliwaagiza wajadili tatizo la uhamiaji
haramu lililopo eneo hilo kwani kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiingia kwenye
bonde hilo bila taarifa kwa kutofuata sheria, kanuni na taratibu, ikiwemo
kukubaliwa na wana kijiji husika.
“Nawaagiza watendaji wa vijiji na kata wa
bonde la Yaeda Chini, hakikisheni hakutokei machafuko tena kwani ninyi mnapokea
mishahara, hivyo fanyeni kazi kwa jasho na kuchukua hatua siyo kusubiri watu wa
wilayani,” alisema Choya.
No comments:
Post a Comment