Saturday 8 September 2012

KONGAMANO LA MADINI,MAFUTA NA GESI

Mchimbaji mdogo Melau Lemunjee akichangia hoja kwenye kikao cha wadau wa madini kilichofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Blue Peal jijini Dar es salaam

1 comment:

  1. WACHIMBAJI wadogo Nchini wametakiwa kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata fursa ya mikopo ya uchimbaji kwani Serikali imetenga zaidi ya sh9.8 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji hao.

    Akizungumza kwenye kongamano la siku tatu la kujadili sekta ya madini,mafuta na gesi lililoanza juzi jijini Dar es salaam,Kaimu Kamishna wa madini Ally Samaje alisema vikundi ndivyo vitawakomboa wachimbaji wadogo.

    Samaje alisema wachimbaji wadogo ambao wataunda vikundi na kuungana watapatiwa fursa ya kuwezeshwa mikopo kwa awamu tofauti kupitia kanda nane za migodi zilizopo kwenye mikoa tofauti hapa nchini.

    “Hatuwezi kutoa mikopo kwa mchimbaji mmoja mmoja kwani baadhi yao wana leseni zilizo mifukoni hivyo japokuwa fedha hizo ni ndogo lakini zitawasaidia kupata vifaa na huduma za migodi yao hivyo waungane,” alisema Samaje.

    Hata hivyo,Mkurugenzi wa Haki Madini Amani Mustafa alipinga suala la kuwashinikiza wachimbaji wadogo waunde vikundi kwani hakuna wachimbaji wadogo walionufaika na kupatiwa mikopo hiyo.

    “Wachimbaji wadogo wanashinikizwa kila mara kuungana ili wapatiwe mikopo na siyo kuungana kwa lengo la kutetea maslahi yao kwani mara nyingi hawatambuliki kutokana na kukosa sauti moja ya kuwatetea,” alisema Mustafa.

    Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini wa mkoa wa Manyara (Marema) Zephania Mungaya alipinga suala la kuwaunganisha wachimbaji hao ili wapate mkopo kwani ushirika migodini hauna tija.

    “Kule Mji mdogo wa Mirerani kuna kikundi cha ushirikia cha uchimbaji madini ya Tanzanite kinachoita Minasco lakini hadi hivi sasa hakuna hatua yoyote ile ambayo wizara ya Nishati na madini imewasaidia,” alisema Mungaya.

    Alisema suala la wachimbaji wadogo kuanzisha vikundi ili wapate mikopo halina tija kwani mara nyingi vikundi hivyo vinakuwa na migogoro isiyo na tija hivyo kuendeleza migogoro na kuwaingiza wachimbaji hao katika sura isiyo nzuri.

    MWISHO.

    ReplyDelete