Wednesday 26 September 2012

WADAU WA MADINI YA TANZANITE

Wadau wa madini ya Tanzanite wakiwa na kikao na Kamanda wa polisi Mkoa wa Manyara,ACP Akili Kupela Mpwapwa

1 comment:

  1. WAMILIKI wa migodi ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wamesema ili ajali zipungue migodini wakutanishwe na kampuni ya TanzaniteOne ambayo huwa inawamwagia maji migodi mwao.

    Waliyasema hayo jana kwenye kikao cha Kamanda wa polisi wa mkoa huo,Akili Mpwapwa na wamiliki hao cha kujadili sababu za kupunguza ajali za mara kwa mara zinazotokea kwenye baadhi ya migodi ya wachimbaji wadogo.

    Sadiki Mnene alisema maji yanayomwagwa na kampuni hiyo ni mengi kama ya elnino na yataweza kuleta maafa kwani hivi karibuni kampuni hiyo ilimwaga maji kwenye mgodi wa Mathias Manga huku wafanyakazi 200 wakiwa mgodini.

    “Haiwezi kuingia akilini kwa watu wasomi kama TanzaniteOne kufanya mambo ya ajabu ya kumwagia maji wachimbaji wadogo badala ya kushirikiana nao dawa tukae nao meza moja tushauriane waache hii tabia,” alisema Mnene.

    Mwenyekiti wa chama cha wachimba madini mkoa wa Manyara Zephania Joseph alisema Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Stephen Masele aliikemea kampuni hiyo isimwage maji lakini walisimama kwa siku mbili tu.

    “Hiyo kampuni haitendi haki kabisa kwani inamwaga maji ambayo yanawaathiri wachimbaji wadogo na sisi tunapotoa taarifa Serikalini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa wakati tupo nchini kwetu,” alisema Joseph.

    Naye,Abubakari Mwamba alisema pamoja na kuwamwagia maji kwenye migodi yao pia baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo wanaingia migodini wakiwa na silaha kinyume na sheria hivyo kuwatia hofu ya wao kulipiza kisasi.

    Diwani wa kata ya Mirerani,Justin Nyari alisema vyombo vya sheria vinatakiwa kutekeleza jukumu lao bila ubaguzi kwa wachimbaji wadogo na wakubwa kuliko hivi sasa wachimbaji wadogo wanaona kuwa mchimbaji mkubwa anabebwa.

    Hata hivyo,akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni,Mwenyekiti wa TanzaniteOne,Ammi Mpungwe alikanusha kuwamwagia maji kwa kudai maji hayo yanatoka yenyewe miambani na kupitia mitobozano ya wachimbaji hao.

    Awali,Mpwapwa alisema kuwa ajali za mara kwa mara zinazotokea kwenye migodi zinamsikitisha kwani tangu Januari mwaka huu hadi jana kulitokea vifo vya watu 18,majeruhi watatu na ajali ya kupoteza viungo mtu mmoja.

    Kwa upande wake,Mkuu wa kituo cha Polisi Mirerani,Ally Mkalipa alisema lengo la kukutana wamiliki wa migodi,maofisa madini na polisi ni kukumbushana majukumu yao ili ajali zinazoweza kuepukika zisitokee.

    MWISHO.

    ReplyDelete