Thursday, 6 September 2012

HAKI MADINI

Mkurugenzi wa Asasi ya Haki Madini Amani Mustafa (kulia) akizungumza jana na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto na Mratibu wa Asasi ya Policy Forum kwenye kongamano la siku tatu la wadau wa madini,mafuta na gesi linalofanyika jijini Dar es salaam na kuhusisha wadau toka mikoa ya Arusha,Manyara,Tanga Mbeya,Iringa na Mwanza

2 comments:

  1. SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati na Madini imetakiwa kutekeleza kwa vitendo sheria mpya ya madini ya mwaka 2010 inayoagiza madini ya vito ikiwemo Tanzanite kuchimbwa na Watanzania wazawa peke kuliko kuwapa wageni.

    Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Kigoma kaskazini Kabwe Zitto (Chadema) kwenye kongamano la kimataifa la kujadili sekta ya madini,mafuta na gesi iliyoanza jana jijini Dar es salaam na kuandaliwa na asasi ya Haki Madini.

    Akizungumza kwenye kongamano hilo Zitto alisema madini ya vito ikiwemo Tanzanite,RubI,Safaya na mengineyo yakichimbwa na watanzania fedha zitabaki hapa nchini na kuingiza faida kwenye jamii kwa ujumla.

    Alisema endapo Serikali itatekeleza uamuzi huo itawafanya wachimbaji wadogo kunufaika kwa kipato na pia watawekeza katika sekta mbali hivyo kuendelea kulipa kodi mbalimbali kutoa ajira zaidi hapa nchini kwa watanzania.

    Alisema kutokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha sheria mwaka 2010 ya madini ya vito kuchimbwa na watanzania peke yao Serikali inatakiwa kutekeleza kwa vitendo sheria hiyo ambayo itawanufaisha watanzania wazawa.

    “Hawa wanapopata madini kwenye machimbo yao wanafaidika wao binafsi na pia wanaingiza mapato kwenye nchi kwani fedha zinabaki hapa hapa kuendeleza nchi tofauti na wageni wanaoondoka nazo,” alisema Kabwe.

    Kwa upande wake,Mkurugenzi wa asasi ya Haki Madini ya mjini Arusha Amani Mustafa alisema lengo la kongamano hilo ni kujenga wigo mpana baina ya wachimbaji wadogo na Serikali ili kutatua vikwazo vinavyowarudisha nyuma.

    Mustafa alisema shabaha ya kongamano hilo siyo kuibua kero na kulalamika peke yake ila ni sehemu ya kuumiza akili na kutafuta majibu ya changamoto zilizopo na kuzitatua kupitia gurudumu moja la safari ya maendeleo.

    Naye,mwandishi wa habari mkongwe Jenerali Ulimwengu alisema Serikali inatakiwa kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo ili wafaidi keki ya Taifa kuliko kuwajali wageni kutoka nje wanaotambulika kwa jina la wawekezaji.

    “Nimetembelea machimbo mengi hapa nchini kama kule Geita na Nzega nimekuta matatizo makubwa kweli kweli wachimbaji wadogo wanafukuzwa na kupewa wageni,hawa ndugu zetu hatuwatendei haki,” alisema Ulimwengu.

    Alisema madini yanapochimbwa na hao wanaoitwa wawekezaji yanazidi kumalizwa hivyo kuacha mashimo makubwa na uharibifu wa mazingira sehemu husika bila kuacha faida yoyote hapa nchini.

    MWISHO.

    ReplyDelete
  2. WACHIMBAJI wadogo Nchini wametakiwa kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata fursa ya mikopo ya uchimbaji kwani Serikali imetenga zaidi ya sh9.8 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji hao.

    Akizungumza kwenye kongamano la siku tatu la kujadili sekta ya madini,mafuta na gesi lililoanza juzi jijini Dar es salaam,Kaimu Kamishna wa madini Ally Samaje alisema vikundi ndivyo vitawakomboa wachimbaji wadogo.

    Samaje alisema wachimbaji wadogo ambao wataunda vikundi na kuungana watapatiwa fursa ya kuwezeshwa mikopo kwa awamu tofauti kupitia kanda nane za migodi zilizopo kwenye mikoa tofauti hapa nchini.

    “Hatuwezi kutoa mikopo kwa mchimbaji mmoja mmoja kwani baadhi yao wana leseni zilizo mifukoni hivyo japokuwa fedha hizo ni ndogo lakini zitawasaidia kupata vifaa na huduma za migodi yao hivyo waungane,” alisema Samaje.

    Hata hivyo,Mkurugenzi wa Haki Madini Amani Mustafa alipinga suala la kuwashinikiza wachimbaji wadogo waunde vikundi kwani hakuna wachimbaji wadogo walionufaika na kupatiwa mikopo hiyo.

    “Wachimbaji wadogo wanashinikizwa kila mara kuungana ili wapatiwe mikopo na siyo kuungana kwa lengo la kutetea maslahi yao kwani mara nyingi hawatambuliki kutokana na kukosa sauti moja ya kuwatetea,” alisema Mustafa.

    Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini wa mkoa wa Manyara (Marema) Zephania Mungaya alipinga suala la kuwaunganisha wachimbaji hao ili wapate mkopo kwani ushirika migodini hauna tija.

    “Kule Mji mdogo wa Mirerani kuna kikundi cha ushirikia cha uchimbaji madini ya Tanzanite kinachoita Minasco lakini hadi hivi sasa hakuna hatua yoyote ile ambayo wizara ya Nishati na madini imewasaidia,” alisema Mungaya.

    Alisema suala la wachimbaji wadogo kuanzisha vikundi ili wapate mikopo halina tija kwani mara nyingi vikundi hivyo vinakuwa na migogoro isiyo na tija hivyo kuendeleza migogoro na kuwaingiza wachimbaji hao katika sura isiyo nzuri.

    MWISHO.

    ReplyDelete