Saturday, 30 December 2017

MAVUNDE AZITAKA TAASISI BINAFSI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WATU WENYE ULEMAVU

Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi,vijana na ajira Anthony Mavunde akimkabidhi fimbo mwenyekiti wa chama cha wasioona mkoa wa Dodoma Omari Lubuva ikiwa ni msaada uliotolewa na Next Generation Microfinance.
Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi,vijana na ajira Anthony Mavunde akiwa na baadhi ya viongozi wa chama cha wasioona mkoa wa Dodoma na meneja wa Next Generation Microfinance wakijaribu kutumia fimbo zilizotolewa na taasisi hiyo kwa ajili ya watu wasioona mkoa wa Dodoma.
Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi,vijana na ajira Anthony Mavunde akizungumza wakati wa kukabidhi fimbo kwa ajili ya watu wasioona mjini Dodoma,kushoto kwake ni mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dodoma Neema Majule na kulia kwake ni meneja wa Next Generation Microfinance Sospeter Kansapa.
Katibu wa chama cha wasioona(TLB)mkoa wa Dodoma Enock Mbawa akizungumza wakati wa kupokea msaada wa fimbo kwa ajili ya watu wasioona,kushoto kwake ni meneja wa Next Generation Microfinance Sospeter Kansapa na kulia kwake ni mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Dodoma Bill Chidabwa.
Meneja wa Next Generation Microfinance Sospeter Kansapa akizungumza wakati wa kukabidhi fimbo kwa ajili ya watu wasioona mkoa wa Dodoma.
Naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi,vijana na ajira Anthony Mavunde akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa jumuiya za CCM mkoa wa Dodoma na wafanyakazi wa Next Generation Microfinance baada ya kukabidhi fimbo kwa ajili ya watu wasioona wa mkoa wa Dodoma.



……………..

NAIBU waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi,Vijana na Ajira Mh Anthony Mavunde leo amekabidhi msaada wa fimbo za kisasa thelathini (30)kwa ajili ya watu wasioona wa mkoa wa Dodoma huku akitoa rai kwa taasisi binafsi na jamii kuweka utaratibu wa kusaidia makundi yenye mahitaji.

Msaada huo umetolewa na taasisi inayojishughulisha na kutoa huduma ya mikopo(NEXT GENERATION MICROFINANCE).

Akikabidhi msaada huo Mavunde ambaye ni mbunge wa Dodoma mjini ameipongeza taasisi hiyo kwa kutumia faida waliyoipata kusaidia watu wenye mahitaji maalum jambo ambalo linapaswa kuwa chachu kwa taasisi nyingine pia.

“Ndugu zanguni mlichokifanya leo kina maana kubwa sio duniani tu bali hata mbinguni,mmeona ni busara kutumia faida mliyoipata kwa ajili ya kusaidia wenzetu wenye mahitaji badala ya kutumia kufanya party,naomba utaratibu huu usiishie leo tu bali muendelee kugusa na makundi mengine yenye uhitaji,”alisema Mavunde.

Katika kusaidia makundi hayo ameiomba pia taasisi hiyo kusaidia chama cha waandishi wa habari wa mkoa wa Dodoma ili waweze kuwa na ofisi yao inayoendana na hadhi ya makao makuu.Ametoa rai pia kwa viongozi wa chama cha wasioona mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanagawa fimbo hizo kwa walengwa bila ya upendeleo wowote.

Akitoa neno la shukrani baada ya kupokea msaada huo katibu wa chama cha wasioona(TLB)mkoa wa Dodoma Enock Mbawa ameishukuru taasisi hiyo kwa kusaidia serikali kupunguza changamoto walizonazo na kuahidi kuhakikisha fimbo hizo zinafika kwa walengwa waliokusudiwa.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi meneja wa Next Generation Microfinance Sospeter Kansapa amesema wameamua kuitikia wito wa rais John Magufuli wa kuwataka wadau wa maendeleo kote nchini kujitokeza kutoa mchango katika ustawi wa Taifa wakiamini kuwa fimbo hizo zitakuwa chachu katika kuleta maendeleo ya Taifa.

No comments:

Post a Comment