Saturday 30 December 2017

KOMBA KAANZA KAZI NA UHAKIKI WA MALI ZA UVCCM MANYARA

 Mwenyekiti wa UVCCM Mkoani Manyara, Mosses Komba akizungumza kwenye kikao cha Baraza la UVCCM Wilayani Hanang.
 Mbunge wa Jimbo la Hanang' Mkoani Manyara, Dkt Mary Nagu akizungumza kwenye kikao cha Baraza la UVCCM Wilayani Hanang.
 Mwenyekiti wa UVCCM Mkoani Manyara, Mosses Komba (wa pili kushoto) baada ya kusimikwa kuwa mzee wa kimila wa Wilaya ya Hanang.

 Mwenyekiti wa UVCCM Mkoani Manyara, Mosses Komba akisaini kwenye kitabu cha wageni, katika ziara yake ya siku moja wilayani Hanang.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoani Manyara, Mosses Komba (wapili kulia) na viongozi wa Wilaya ya Hanang' wakiwa tayari kuanza kikao cha Baraza la UVCCM Wilayani humo.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoani Manyara, Mosses Komba  amesema ameanza majukumu ya utekelezaji wa nafasi hiyo hiyo kwa kufanya uhakiki na kufuatilia mali za jumuiya hiyo ikiwemo jengo na gari.

Komba aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la UVCCM wilayani Hanang' kilichofanyika mji mdogo wa Katesh.

Komba alisema jengo la UVCCM mkoa huo lililokuwa linatumika kama mahakama ya wilaya ya Babati, hivi sasa limesharudi mikononi mwao na wanatarajia kuhamia hapo wakati wowote kuanzia sasa.

Alisema gari la jumuiya hiyo lililokuwa jijini Arusha kwa matengenezo amefuatilia mahali lilipo hivyo wapo kwenye mchakato wa kulirudisha mjini Babati.

Alisema ameunda tume yenye wajumbe watatu akiwemo katibu wa UVCCM mkoani humo Raphael Sumaye, Kudra Bura wa Babati na Hashim Idd wa Kiteto na yeye mwenyewe atakuwa anaiongoza tume hiyo ili kuhakiki mali za jumuiya hiyo.

"Ili kuhakikisha tunafanikisha kufuatilia mali za UVCCM Manyara, nimeunda tume hiyo ya watu watatu watakaohakiki mali za UVCCM mkoa Manyara kwa kupita kwenye kila wilaya," alisema Komba.

Mbunge wa Jimbo la Hanang Dk Mary Nagu alisema wanachama wa CCM Mkoa wa Manyara, wamewachagua viongozi wa kutoka wilaya zote za mkoa huo bila kubagua ukanda wala ukabila.

Dk Nagu alisema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Simon Lulu ametokea wilaya ya Mbulu, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa Mosses Komba ni mkazi wa wilaya ya Simanjiro, Mwenyekiti wa UWT Venossa Mjema ametokea wilaya ya Hanang, na Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi Fraiten Qwaison ametokea wilaya ya Kiteto.

Alisema ili kuonyesha mshikamano kwenye mkoa huo, mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM ngazi ya Taifa (Mnec) Joachim Leonce ametokea eneo la Dareda wilaya ya Babati, Katibu wa siasa, uenezi na itikadi Jacob Siay ni mkazi wa Babati mjini na mjumbe wa baraza kuu la UWT Taifa, Magreth Maina ametokea wilayani Hanang.

Mjumbe wa Baraza la UVCCM Wilayani Hanang' Caroli Gisimoy alisema vijana wengi bado ni wachanga kwenye jumuiya hiyo hivyo wanapaswa kupata semina na mafunzo mbalimbali ili wajengewe uwezo zaidi.

Gisimoy alisema vijana hao hasa viongozi wa jumuiya hiyo kwenye kati ya kata 33 za wilaya hiyo wanapaswa kupatiwa elimu ili waweze kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Katibu wa UVCCM mkoani Manyara, Raphael Sumaye alisema amefurahishwa na kasi kubwa ya utekelezaji majukumu yake iliyoonyeshwa na Mwenyekiti huyo hivyo naye yupo tayari kwenda naye sambamba.

"Vijana tunapaswa kwenda sambamba na kasi ya Mwenyekiti wetu Komba, kwani anashabihiana na kasi ya Rais John Magufuli na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Heri James," alisema Sumaye.

No comments:

Post a Comment