Friday 22 December 2017

MADINI YA TANZANITE YA SHILINGI BILIONI 1.84 YAUZWA KWENYE MNADA

 Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Shirika la madini la Taifa, Stamico, Alexander Muganda akizungumza kwenye mnada wa madini wa madini ya Tanzanite. 
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akizungumza kwenye mnada wa madini ya Tanzanite. 
 Wadau wa madini ya Tanzanite wakiwa kwenye mnada wa madini hayo. 
 Wadau wa madini ya Tanzanite wakiwa kwenye mnada wa madini hayo. 
 ndNaibu Waziri wa Madini Ladslaus Nyongo na viongozi mbalimbali wakizungumza mawili matatu kwenye mnada huo 
 Wadau wa madini ya Tanzanite na askari polisi wakiwa kwenye mnada wa madini hayo. 
Kamishna wa madini nchini mhandisi Benjamin Mchwampaka akitoa taarifa ya mnada wa madini ya Tanzanite. 

Madini ya shilingi bilioni 1.84 yauzwa kwenye mnada wa Tanzanite

Madini ghafi ya Tanzanite yenye thamani ya shilingi bilioni 1.84 bilioni yameuzwa kwenye mnada wa tatu wa kimataifa wa madini uliofanyika mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Kamishna wa madini nchini, mhandisi Benjamini Mchwampaka akizungumza  kwenye ufungaji wa mnada huo alisema madini hayo yametokana na jumla ya gramu 47,201 zilizouzwa.

Mhandisi Mchwampaka alisema awali, kampuni tatu zilileta madini yao kuuzwa kwenye mnada huo lakini kampuni mbili zilijitoa.

 Alitaja kampuni hizo ni TanzaniteOne kwa kushirikiana na shirika la madini nchini (Stamico) ambao wana ubia wa asilimia 50 kwa 50, kampuni ya Tanzanite Africa na Clasic Gems.

Alisema kampuni hizo zilileta madini hayo kwa ajili ya kuuzwa kiasi cha gramu 52,146.62 za madini ghafi ya Tanzanite na kampuni ya Classic Gems ilileta karati 697.26 kwa ajili ya mauzo.

Alisema kampuni mbili za Tanzanite Africa na Classic Gems zilijitoa kwenye mnada huo baada ya kutoridhika na bei iliyotolewa hivyo madini yaliyouzwa ni ya kampuni ya TanzaniteOne na Stamico.

Kamishna huyo alisema Serikali inatarajia kulipwa shilingi milioni 128.7 za mrabaha na ada ya ukaguzi na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro inatarajia kulipwa shilingi milioni 5 za kodi ya huduma.

“Kampuni 60 kutoka nchi saba za Tanzania, Marekani, Sri-Lanka, Hong Kong, India, Thailand  na China, zilishiriki kwenye mnada huo,” alisema mhandisi Mchwampaka.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Stamico, Alexander Muganda alisema mnada huo wa kwanza umekuwa na mafanikio kama walivyotarajia.

"Tunashukuru Rais Magufuli kwa agizo lake la kufanyia mnada eneo hilo la Mirerani ambapo ndipo madini hayo yanapatikana," alisema Muganda.

Naibu Waziri wa Madini, Ladslaus Nyongo alisema serikali ya awamu ya tano imeonyesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa rasilimali zinawanufaisha watanzania kwa kiwango cha juu kabisa.

Nyongo alisema tangu mwaka 2011 serikali ilianza utaratibu wa kutoa cheti cha uhalisia kwa madini ya Tanzanite yanaposafirishwa kwenda nje kwa utaratibu halali za serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alipongeza hatua ya kuweka mnada wa madini ya Tanzanite sehemu ambayo yanachimbwa kama Rais John Magufuli alivyoahidi.

Mnyeti alisema serikali ya awamu ya tano itahakikisha inakusanya kodi kwa wachimbaji wengine wa madini ya Tanzanite na siyo kuibana kampuni ya TanzaniteOne pekee.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula alitoa shukurani nyingi kwa Rais John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuagiza madini ya Tanzanite yafanyiwe mnada kwenye mji mdogo wa Mirerani.

“Tunakumbuka ahadi yake Rais Magufuli aliyoitoa wakati akizindua barabara ya lami ya Kia-Mirerani kuwa minada yote ya madini ya Tanzanite yafanyike katika machimbo haya ya Tanzanite na hilo limetekelezwa tunashukuru sana,” alisema mhandisi Chaula.

Mkurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne, Hussein Gonga alisema anashukuru uamuzi wa Rais John Magufuli kuagiza mnada wa madini kufanyika eneo linalochimbwa madini hayo.

Gonga alisema jamii inayozunguka eneo hilo imenufaika kupitia mnada huo kwa kufanya biashara mbalimbali kwa wadau wa madini ikiwemo nyumba za kulala wageni, vyakula, vinywaji na mengineyo.



No comments:

Post a Comment