Tuesday, 6 June 2017

WALIA NA MPAKA WA EPZ

Baadhi ya watu wanaopakana na eneo huru la biashara la uwekezaji la (EPZ) Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameiomba Serikali kubainisha mpaka kwani uliopo umeingilia sehemu yao.
 
 Wakazi hao wanadai kuwa mpaka halali wa eneo la EPZ ni hekta 510.64 na siyo hekta 530.87 kama zinavyobainishwa kwani mpaka uliokuwepo awali unaonyesha hivyo na vibao vipo hadi hivi sasa.
 
Wakizungumza jana, wananchi hao walidia kuwa walifikisha kilio chao kwa Waziri mkuu Kasimu Majaliwa alipofanya ziara yake mkoani Manyara,  mwezi Februari mwaka huu na kufika Mirerani.
 
Mchungaji Michael Mtero alisema Waziri mkuu Majaliwa alimuagaiza mkuu wa mkoa huo Dk Joel Bendera afuatilie mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi hivyo wanahitaji kujua hatima ya suala hilo.
 
“Mimi nilipatiwa eneo hili ili nijenge kanisa na muumini mmoja ambaye alijitolea sadaka kiwanja chake ila naambiwa kuwa sehemu ya uwanja ipo katika mpango wa EPZ,”  alisema mchungaji Mtero.
 
Blasto Mosses alisema alijenga nyumba baada ya kuuziwa eneo hilo na kupata nyaraka halali kutoka serikalini lakini anashangazwa kuambiwa kuwa nyumba na kiwanja kipo ndani ya sehemu ya EPZ.
 
Israel Loserian alisema hivi sasa wameshikwa na sintofahamu ya tatizo hilo kwani ni muda mferu walikuwa wanamiliki maeneo yao na hivi karibuni kuambiwa kuwa wapo ndani ya uwekezaji wa EPZ.
 
Michael Lekopito (95) alisema alizaliwa kwenye eneo hilo lakini anashangazwa kuambiwa kuwa wamevamia sehemu hiyo ambayo hawakulipwa fidia yao kama baadhi ya watu walivyolipwa.
 
Hata hivyo, mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula alisema waliopo kwenye eneo hilo wapo kimakosa kwani mpaka unaonyesha kuwa wameingia ndani ya na walishawaambia waondoke wenyewe.
 
Mhandisi Chaula alisema walishawaeleza waliouziwa sehemu hiyo wabomoe, kwani awali serikali ilileta mpimaji wakagoma, wakamleta mpima wao akasema wapo ndani ya eneo, hata fedha hawakumlipa.
 
“Hivi sasa wizara ya Nishati na Madini inatarajia kujenga jengo lao kubwa la madini house kwenye eneo hilo na pia tunatarajia kuweka mtaro ili kubainisha vizuri mpaka wa EPZ,” alisema mhandisi Chaula.

No comments:

Post a Comment