Thursday 15 June 2017

WATANZANIA WATAKIWA KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI KWENYE VITA YA KULINDA RASILIMALI



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga amesema watanzania wanapaswa kumuunga mkono Rais John Magufuli kwenye vita ya kulinda rasilimali za nchi aliyoianzisha.

Kamoga aliyasema hayo juzi kwenye maadhimisho ya siku ya albino
duniani, ambayo  kimkoa ilifanyika kituo cha 4 Angle mji mdogo wa
Haydom na alimwakilisha mkuu wa mkoa huo Dk Joel Bendera.

Alisema vita ya kulinda rasilimali ya nchi inapaswa kuungwa mkono
kwani utajiri wa nchi ya Tanzania haulingani na hali halisi iliyopo
kutokana na watu wachache kupora utajiri kupitia madini mbalimbali.






Alisema ana imani Rais Magufuli na watanzania kwa ujumla watashinda vita ya kulinda rasilimali kwani kupitia ripoti ya pili ya makania imeonyesha namna wananchi wanyonge wanavyoibiwa.

“Pamoja na kuathimisha siku ya albino duniani tunapaswa kumuunga mkono Rais Magufuli katika vita hii ya kusimamia na kulinda rasilimali za nchi kupitia madini yetu kwani nia ya dhati ameionyesha,” alisema Kamoga.



 

Mwenyekiti wa chama cha maalbino mkoani Manyara, Joseph Masasi alisema wanakabiliwa na changamoto ya kutobaini idadi kamili ya watu wenye ualbino mkoani humo hivyo kukosa takwimu sahihi.

Masasi alisema tatizo hilo linasababisha hata kukitokea tatizo lolote
linalohitaji msaada kwao inakuwa vigumu kwani wengine wanakosa
kutokana na kutobainishwa kwa idadi yao katika wilaya za mkoa huo.

Alisema pia wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa mafuta maalum ya
kujipaka kwa watu wenye ualbino yanayowasaidia kila siku ili
wasiathiriwe na mionzi ya jua na kusababisha baadhi yao kuathirika.

“Pamoja na hayo tunashukuru kwenye mkoa wa Manyara hakuna matukio ya watu wenye ualbino kuuawa au kukatwa viungo na watu makatili ila kuna badhi ya matishio madogo madogo,” alisema Masasi.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Joseph Mandoo alisema halmashauri yao itaendelea kushirikiana na uongozi wa ualbino kwa ajili ya kuhakikisha wanatoa msaada unaohitajika kwa watu hao.

Mandoo alitoa wito kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye ualbino kutowafisha ndani na badala yake wawafikishe kwenye sehemu husika ili pindi misaada itakapotolewa waweze kupatiwa.




No comments:

Post a Comment